Miripuko pacha ya mabomu yaua watu kadhaa mjini Mogadishu, Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115364-miripuko_pacha_ya_mabomu_yaua_watu_kadhaa_mjini_mogadishu_somalia
Kwa akali watu wanane wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika miripuko pacha ya mabomu iliyotokea katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu.
(last modified 2026-05-13T14:18:38+00:00 )
Aug 18, 2024 08:43 UTC
  • Miripuko pacha ya mabomu yaua watu kadhaa mjini Mogadishu, Somalia

Kwa akali watu wanane wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika miripuko pacha ya mabomu iliyotokea katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu.

Mohamud Ahmed, afisa wa polisi mjini Mogadishu amesema, shambulio hilo limelenga duka la chai katika wilaya ya Daynile.
 
"Duka la chai lilikuwa na shughuli nyingi wakati wa miripuko. Tunaamini kuwa bomu lilikuwa limetegwa ndani ya duka la chai," ameeleza afisa huyo wa polisi.
 
Kwa mujibu wa Ahmed, duka hilo hutembelewa mara kwa mara na wenyeji we eneo hilo na baadhi ya askari wa vyombo vya usalama wanaofanya kazi hapo; lakini hakuthibitisha au kukanusha kama askari wa usalama walikuwa miongoni mwa waliouawa au kujeruhiwa.
Wanamgambo wa Al-Shabab

Hakuna kundi lililodai kuhusika na miripuko hiyo ambayo ilitokea jana Jumamosi.

Siku ya Ijumaa pia watu wasiopungua 12 waliuawa wakati gari lililokuwa limebeba wanajeshi lilipokanyaga bomu lililotegwa ardhini katika jimbo la Kusini Magharibi.

Mnamo Agosti 3, watu wapatao 37 waliuawa katika shambulio la bunduki lililotokea kwenye ufukwe maarufu katika mji mkuu wa Somalia.

Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi la Al Shabab limekuwa likipambana na Serikali ya Somalia na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika.

Al Shabab imeongeza mashambulizi tangu Rais Hassan Sheikh Mohamud alipotangaza kuanzishwa "vita kamili vya pande zote" dhidi ya kundi hilo la kigaidi.../