Abdul-Fatah al-Burhan kuunda serikali ya mpito Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115382-abdul_fatah_al_burhan_kuunda_serikali_ya_mpito_sudan
Mkuu wa Baraza la Utawala wa Sudan, Abdel Fattah Al-Burhan ametangaza habari ya kuweko juhudi za kuunda serikali ya mpito katika nchi hiyo inayosumbuliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 18, 2024 23:21 UTC
  • Abdul-Fatah al-Burhan kuunda serikali ya mpito Sudan

Mkuu wa Baraza la Utawala wa Sudan, Abdel Fattah Al-Burhan ametangaza habari ya kuweko juhudi za kuunda serikali ya mpito katika nchi hiyo inayosumbuliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Haya yanajiri takriban miaka 3 baada ya Al-Burhan kuvunja serikali ya kiraia iliyobuniwa kuiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha mpito kufuatia kuondolewa madarakani Rais Omar Al-Bashir mwaka 2019.

Jenerali Al-Burhan amesema hayo katika mkutano wake na ujumbe wa vyombo vya habari vya "Sudan na Misri na kueleza kwamba "yeyote anayetaka kusimamisha vita lazima azungumze na waasi wanaoshambulia raia katika maeneo yao."

Amesisitiza kuwa, ukiukwaji unaofanywa na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka dhidi ya watu wa Sudan haujawahi kutokea katika vita vyote duniani, akisisitiza kuwa waligawanya makabila hayo na kutaka kuunda mpasuko wa kijamii miongoni mwao.

Aliongeza: "Msimamo wa serikali juu ya mazungumzo yoyote unajulikana kupitia dira iliyowasilishwa kwa wapatanishi. Serikali pia iko wazi katika mipango yoyote inayojitolea kwa uhuru na uadilifu wa eneo la Sudan na utekelezaji wa maamuzi ya Mkataba wa Jeddah."

Sudan imekumbwa na vita kati ya jeshi, linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye ni mkuu wa Baraza la Mpito la Utawala, na kundi la RSF linaloongozwa na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, takriban watu 12,260 wameuawa na zaidi ya 33,000 kujeruhiwa katika vita vilivyoanza Aprili 2023,

Mgogoro wa kibinadamu unaendelea kuwa mbaya zaidi kwani karibu watu milioni 6.8 wamekimbia makazi yao kutafuta usalama nchini Sudan au nchi jirani. Jitihada za kieneo na kimataifa hadi sasa ziimeshindwa kukomesha mapigano hayo.