Algeria kuharakisha kupeleka mafuta Lebanon ili kupunguza mgogoro wa umeme
Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria ameamuru kupelekwa haraka mafuta nchini Lebanon ambayo imekumbwa na uhaba mkubwa wa umeme.
Hayo yametangazwa na redio ya serikali ya Algeria na kuongeza kuwa, uamuzi huo umewasilishwa na Waziri Mkuu wa Algeria, Nadir Larbaoui kwa Waziri Mkuu wa Lebanon, Najib Mikati.
Larbaoui amemhakikishia Mikati kwamba shehena ya mafuta ya Algeria itakayopelekwa Lebanon inaakisi dhamira ya Algiers ya kuisaidia Lebanon katika nyakati hizi zenye changamoto, kuviwezesha vituo vya kuzalisha umeme vya Lebanon kuendelea na kazi yake na kusaidia kurejesha gridi yake ya umeme katika mkondo wake.
Pia jana Jumapili, ofisi ya Waziri Mkuu wa Lebanon ilitoa taarifa iliyosema kuwa, Mikat ameishukuru nchi ndugu ya Algeria kwa uamuzi wake huo na kuiomba Algiers iendelea kuwa pamoja na Lebanon katika nyanja zote.
Gridi ya umeme ya Lebanon imezimwa kabisa baada ya mtambo wake wa mwisho unaofanya kazi kukosa mafuta, hivyo kutatiza miundombinu muhimu kote nchini humo, ikiwa ni pamoja na viwanja vya ndege, bandari, pampu za maji, mifumo ya maji taka na magereza.
Uhaba wa vifaa umewaacha wakaazi wengi wa Lebanon kutegemea jenereta ya watu binafsi na paneli za jua kujizalishia umeme.