Sudan yatuma wajumbe mjini Cairo kukutana na wapatanishi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115410-sudan_yatuma_wajumbe_mjini_cairo_kukutana_na_wapatanishi
Serikali ya Sudan imetuma wajumbe wake mjini Cairo kwa majadiliano juu ya ushiriki wake katika mazungumzo ya amani yenye lengo la kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miezi 16 nchini humo.
(last modified 2024-08-19T08:32:17+00:00 )
Aug 19, 2024 08:32 UTC
  • Sudan yatuma wajumbe mjini Cairo kukutana na wapatanishi

Serikali ya Sudan imetuma wajumbe wake mjini Cairo kwa majadiliano juu ya ushiriki wake katika mazungumzo ya amani yenye lengo la kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miezi 16 nchini humo.

Serikali ya Sudan imesisitiza kuwa haitahudhuria mazungumzo ya amani yanayoongozwa na Marekani nchini Uswizi hadi pale makubaliano ya awali yaliyokubaliwa mjini Jeddah yatakapotekelezwa.

Taarifa ya Baraza la Mpito la Utawala nchini Sudan linaloongozwa na mkuu wa jeshi Jenerali Abdul Fattah El Burhan ilisema kuwa uamuzi wa kwenda Cairo umekuja baada ya mawasiliano na wapatanishi kwa lengo la kujadili utekelezaji wa makubaliano ya Jeddah. Chini ya makubaliano hayo wanamgambo wa RSF wanaopigana na jeshi wanapaswa kuondoka katika maeneo ya kiraia.

Vyanzo vya ngazi ya juu vya serikali viliwaambia waandishi wa habari kwamba serikali imewasilisha maono yake kuhusu hilo na mada nyinginezo kwa wapatanishi na kusisitiza kwamba mbinu yake ya mazungumzo zaidi itatokana na majibu yao. Vyanzo hivyo vimekanusha ripoti za vyombo vya habari kwamba serikali tayari imetuma ujumbe Geneva.

Mahasimu wawili wakuu katika vita vya Sudan, Abdel Fattah al-Burhan (kushoto) na  Mohamed Hamdan Daglo

Jambo lingine ambalo serikali ya Sudan inalipinga vikali ni uwepo wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) katika mazungumzo ya amani. Wakuu wa Sudan wanaituhumu UAE kuwa inaunga mkono wanagambo wa RSF, madai ambayo UAE imeyakanusha. Wataalamu wa Umoja wa Mataifa, hata hivyo, wamesema kuna ushahidi kuwa UAE inaunga mkono waasi wa RSF ambao wanatekeleza jinai katika maeneo kadhaa ya Sudan hasa Darfur.

Nchi hiyo ya kaskazini-mashariki mwa Afrika imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu Aprili 2023 kati ya jeshi la Sudan chini ya mtawala mkuu wa nchi hiyo, Abdel Fattah al-Burhan, na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), kinachoongozwa na makamu wake wa zamani, Mohamed Hamdan Daglo.