Wapinzani Malawi wampitisha tena Mutharika kuwania kiti cha urais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115414-wapinzani_malawi_wampitisha_tena_mutharika_kuwania_kiti_cha_urais
Chama kikuu cha upinzani nchini Malawi cha Democratic Progress kimempasisha rais wa zamani Peter Mutharika kuwa mgombea wake katika uchaguzi wa rais hapo mwakani.
(last modified 2024-08-19T22:42:25+00:00 )
Aug 19, 2024 22:42 UTC
  • Wapinzani Malawi wampitisha tena Mutharika kuwania kiti cha urais

Chama kikuu cha upinzani nchini Malawi cha Democratic Progress kimempasisha rais wa zamani Peter Mutharika kuwa mgombea wake katika uchaguzi wa rais hapo mwakani.

Mutharika mwenye (84), ambaye alikuwa rais wa malawi kuanzia mwaka 2014 hadi 2020, amesema katika hotuba yake kwamba yeye na chama chake watarekebisha na kuboresha hali ya uchumi, ambayo imeshuhudia ukuaji mdogo na uhaba wa sarafu za kigeni vilivyosababisha ukosefu wa mafuta na dawa.

Peter Mutharika anatarajiwa kuchuana na Rais wa sasa Lazarus Chakwera wa chama cha Malawi Congress anayewania muhula wa pili katika uchaguzi mkuu ujao.

Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) hivii karibunii ilichapisha ratiba ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo ambao umepangwa kufanyika Septemba 16, 2025.

Rais wa sasa wa Malawi Lazarus Chakwera

 

Mwenyekiti wa MEC, Jaji Annabel Mtalimanja amesema kuwa tume yake itafanya zoezi la uandikishaji wapiga kura kuanzia mwezi Septemba hadi Disemba mwaka huu katika awamu tatu za siku 14-14 kote nchini humo.

kwa sasa, tume hiyo inashirikiana na Ofisi ya Taifa ya Usajili wa Vitambulisho ya Malawi (NRB), ili kuhakiksha kuwa, kila raia wa Malawi mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea, au chini ya miaka 18, lakini atakuwa amefikia miaka 18 ifikapo siku ya uchaguzi, anapata kitambulisho cha taifa.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Malawi itatangaza ada watakazotozwa wagombea wakati wa kujiandikisha na kwamba karatasi za uteuzi wa wagombea wa serikali za mitaa, ubunge na urais zitatolewa katika miezi ya Aprili, Mei na Juni mfululizo.