TEC: Kutowasikiliza wamasai wa Ngorongoro Tanzania ni kuwanyima haki zao
Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania (TEC) limesema kutowasikiliza Wamaasai wanaioshi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ni kuwanyima haki zao.
Kauli hiyo inakuja wakati mamia ya vijana na akina mama wa eneo hilo walipoandamana juzi wakiishinikiza Serikali kuwapa huduma za mbalimbali za kijamii.
Akizungumza jana, Katibu wa TEC Padri Charles Kitima alisema, "Leo hii tunapozungumza ndugu zetu Wamasai wa kule Ngorongoro wanatuma ujumbe mbaya wenye twasira hasi Kimataifa… “…unapowaeleza ni hiari yao kubaki Ngorongoro halafu ukawanyima haki zao za msingi huo ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Juzi Jumapili maandamano ya amani yaliyofanywa na jamii ya Wamasai ambayo yalidumu kwa masaa kadhaa huku shughuli za utalii zikilazimika kusimama.
Watetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania pia wamezitaka mamlaka za Tanzania kuheshimu haki za jamii hiyo kwa kusikiliza na kuwapa mahitaji yao ya msingi.
Tangu mwaka 2022, Mamlaka nchini Tanzania zimekuwa zikiendesha zoezi la kuhamisha watu kutoka eneo hilo la hifadhi kwenda kwenye eneo la Msomera mkoani Tanga.
Hata hivyo, tangu kuanza kwa zoezi hilo takribani watu 7,000 wameshahama kwa hiari huku baadhi wakieleza kutokuwa tayari kuhama.
Mwaka 2010, eneo la hifadhi ya Ngorongoro lilitambuliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO kuwa eneo la urithi wa dunia.