Somalia yamkosoa vikali  Balozi wa Uingereza kwa kuibua mifarakano
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115428-somalia_yamkosoa_vikali_balozi_wa_uingereza_kwa_kuibua_mifarakano
Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia Ahmed Moalim Fiqi amemkosoa vikali Balozi wa Uingereza nchini Somalia, Mike Nithavrianakis, kwa matamshi aliyoyataja kuwa "mashambulizi ya wazi dhidi ya mamlaka na umoja wa Somalia."
(last modified 2024-08-20T03:27:11+00:00 )
Aug 20, 2024 03:27 UTC
  • Somalia yamkosoa vikali  Balozi wa Uingereza kwa kuibua mifarakano

Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia Ahmed Moalim Fiqi amemkosoa vikali Balozi wa Uingereza nchini Somalia, Mike Nithavrianakis, kwa matamshi aliyoyataja kuwa "mashambulizi ya wazi dhidi ya mamlaka na umoja wa Somalia."

Mzozo wa kidiplomasia umeibuka baada ya Balozi Nithavrianakis kuchapisha maoni kwenye ukurasa wake wa X (zamani Twitter), ambayo Waziri Fiqi amesema yanahujumu mamlaka ya mipaka ya Somalia.

Katika ujumbe wake,  Balozi Nithavrianakis, ameonyesha fahari yake kuwa Uingereza inaunga mkono kazi ya shirika lisilo la kiserikali la HALO Trust nchini Somalia na Somaliland. HALO Trust, ni shirika lenye makao yake nchini Uingereza linalojihusisha na uteguaji mabomu.

Waziri Fiqi hakumung’unya maneno katika majibu yake, akilaani matamshi ya balozi huyo kuwa hayakubaliki.

"Kuibua mgawanyiko katika nchi  na kuarifisha majina mawili tofauti ni jambo lisilokubalika kabisa na ni shambulio la wazi dhidi ya mamlaka na umoja wa Somalia."

Kauli yake inaakisi msimamo wa muda mrefu wa serikali ya Somalia kuhusu suala la Somaliland, eneo ambalo lilijitangazia uhuru wake kutoka kwa Somalia mwaka 1991 lakini bado halijatambuliwa kimataifa kama taifa huru.

Uingereza inaonekana kuchochea kujitenga Somaliland kwa sababu eneo hilo lilikuwa chini ya himaya yake katika zama za ukoloni wakati maeneo mengine ya Somalia yalikuwa chini ya himaya ya Italia. Maeneo yote ya Somalia yaliungana baada ya uhuru kabla ya Somaliland kutangaza kujitenga mwaka 1991.