Sudan na Russia kutumia sarafu za ndani katika shughuli za kibiashara
Ujumbe kutoka Benki Kuu ya Russia umetembelea Sudan ili kujadiliana na Gavana wa Benki Kuu ya nchi hiyo, Borai al-Siddiq, kuhusu matumizi ya sarafu za nchi hizo mbili katika miamala ya kibiashara ili kupunguza utegemezi wa sarafu za kigeni hasa dola ya Marekani.
Kulingana na shirika rasmi la habari la nchi hiyo, SUNA, ujumbe wa Russia pia umejadili fursa za uwekezaji wa pamoja katika sekta muhimu kama vile madini ya thamani, ikiwa ni pamoja na dhahabu. Benki za Sudan na Russia zinatarajiwa kuwa na uwezo wa kufadhili miradi hii.
Ufunguzi wa matawi ya benki katika nchi hizo mbili utasaidia mabadilishano ya biashara na kuongeza mauzo ya nje na uagizaji pia unazingatiwa.
Katika Kongamano la 27 la Kimataifa la Kiuchumi la Saint Petersburg nchini Russia, nchi wanachama wa BRICS zilitangaza tena utayari wa kutekeleza kivitendo hatua ya kuunda sarafu moja ya kidijitali.
Nchi za BRICS, zikiiongozwa na Russia zinajaribu kuimarisha utawala wao wa kifedha na kujikinga na athari hasi za vikwazo vya Magharibi hasa Marekani kwa kupunguza utegemezi wa dola ya Marekani na kupitisha mbinu mbadala za malipo.