Burkina Faso, Mali, Niger zaishutumu Ukraine kwa kuunga mkono ugaidi Sahel
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115464-burkina_faso_mali_niger_zaishutumu_ukraine_kwa_kuunga_mkono_ugaidi_sahel
Burkina Faso, Mali na Niger zimewasilisha ombi kwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili lilaani waziwazi kitendo cha Ukraine cha kuunga mkono ugaidi wa kimataifa" hasa katika eneo la Sahel Afrika.
(last modified 2024-08-21T03:19:45+00:00 )
Aug 21, 2024 03:19 UTC
  • Burkina Faso, Mali, Niger zaishutumu Ukraine kwa kuunga mkono ugaidi Sahel

Burkina Faso, Mali na Niger zimewasilisha ombi kwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili lilaani waziwazi kitendo cha Ukraine cha kuunga mkono ugaidi wa kimataifa" hasa katika eneo la Sahel Afrika.

Hatua hiyo imekuja baada ya matamshi ya hivi karibuni ya maafisa wa Ukraine waliotangaza hadharani kuwa Kyiv ilihusika katika mashambulizi ya waasi waTuareg wanaotaka kujitenga na kusababisha mauaji ya wanajeshi wengi wa Mali mwezi uliopita. Mauaji hayo dhidi ya wanajeshi wa serikali ya Mali yalifanyika katika kijiji cha Tinzawaten cha kaskazini mashariki mwa Mali karibu na mpaka wa nchi hiyo na Algeria.

Katika barua ya pamoja, mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo tatu za Burkina Faso, Mali na Niger wamesema kuwa, nchi zao zilishangazwa na matamshi ya kijeuri ya Andriy Yusov, msemaji wa idara ya ujasusi ya jeshi la Ukraine ambaye alikiri hadharani kuwa nchi yake ilihusika moja kwa moja katika mashambulizi ya kiwoga, kinyama na kijinai dhidi ya wanajeshi wa Mali kati ya Julai 24 na 26 mwaka huu.

Wanajeshi vamizi wa Marekani katika eneo la Sahel

 

Taarifa ya nchi hizo tatu za magharibi mwa Afrika imeongeza kuwa, matamshi hayo yalithibitishwa na kutiliwa mkazo na Yurii Pyvovarov, balozi wa Ukraine nchini Senegal.

Barua hiyo imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua zinazofaa dhidi ya vitendo hivyo vya uasi vya Ukraine vinavyoimarisha magenge ya kigaidi barani Afrika.

Barua hiyo pia imesema: "Huu ni msaada rasmi na usio na shaka wa serikali ya Ukraine kwa ugaidi barani Afrika, haswa katika eneo la Sahel. Vitendo hivi pia vinajumuisha ukiukaji wa mamlaka ya kujitawala mataifa yetu. Huo ni uchokozi wa wazi na uungaji mkono kwa ugaidi wa kimataifa, ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na mikataba ya kimataifa inayohusika."