Wito wa kimataifa wa kutekeleza "Azimio la Jeddah" kuhusu Sudan
Washirika wa kimataifa katika mazungumzo ya Geneva wametoa wito kwa pande zote mbili za vita nchini Sudan kutekeleza ahadi zilizotolewa katika Azimio la Jeddah zaidi ya miezi 3 iliyopita.
Wito huo umetolewa katika taarifa ya pamoja ya Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa, Misri, Saudi Arabia, Uswisi, Marekani na Imarati kuhusu mazungumzo ya Geneva, ambayo yalizinduliwa Jumatano iliyopita mbele ya wajumbe wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) na serikali ya Sudan.
Kabla ya mazungumzo yoyote mapya ya kumaliza vita vya ndani huko Sudan, serikali ya Khartoum imeshurutisha utekelezaji wa "Azimio la Jeddah," ambalo lilitolewa Mei 2023 katika hitimisho la majadiliano yaliyoandaliwa katika mji wa Jeddah huko Saudia kati ya jeshi la serikali ya Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka.
Azimio hilo lilizitaka pande zote mbili kwenye vita "kujiepusha na mashambulizi ya kijeshi ambayo yanaweza kusababisha madhara kwa raia," na "kuheshimu sheria za kibinadamu na za kimataifa za haki za binadamu."
Taarifa hiyo imeongeza kuwa wajumbe hao walisisitiza udharura wa kukidhiwa mahitaji ya dharura ya kibinadamu ya watu wa Sudan, kuheshimiwa sheria za kimataifa za kibinadamu, na kutekelezwa Azimio la Jeddah.
Mazungumzo ya amani Sudan yalizinduliwa mjini Geneva Jumatano iliyopita mbele ya wawakilishi wa washirika wa kimataifa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na serikali ya Sudan.