Utapiamlo wa watoto wafikia kiwango cha juu zaidi nchini Mali
Nchini Mali, shirika lisilo la kiserikali la Action Against Hunger linabainisha ongezeko la kutisha la visa vya utapiamlo wa watoto katika ripoti iliyochapishwa hivi karibuni. Watoto walio na umri wa chini ya miaka 5 wanaoishi ndani ya kambi za wakimbizi kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo wameathirika zaidi.
Utapiamlo huathiri asilimia 30 ya watoto katika baadhi ya maeneo. Miongoni mwa sababu za utapiamlo huu wa watoto zilizotajwa na shirika hilo ni migogoro mbalimbali nchini Mali inayoendelea tangu mwaka 2012.
Nchini Mali, ongezeko la utapiamlo miongoni mwa watoto linaweza kuelezewa kwa kiasi fulani kutokana na migogoro mbalimbali ambayo imetokea nchini Mali tangu mwaka 2012. Haya yamewalazimu watu kukimbia, na kuacha majukumu yao yote ya kujikimu, hali inayozidi kuwa mbaya, kulingana na shirika la kimataifa la Action Against Hunger (ACF) katika ripoti iliyochapishwa hivi karibuni.
Kulingana na Mamadou Diop, mkurugenzi wa nchi wa Action Against Hunger nchini Mali, "tumefikia viwango vya utapiamlo ambavyo havijawahi kuwa sawa katika miaka 10 iliyopita, vya 30% ya utapiamlo mkali duniani. Na kiwango kikubwa cha utapiamlo cha 11%, ikifahamika kwamba kizingiti cha tahadhari ni 2% kwa utapiamlo mkali.
Serikali ya mpito ya kijeshi iliingia madarakani nchini Mali mnamo Mei 2021 kupitia mapinduzi ya kijeshi. Disemba mwaka jana, Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa huko Mali (MINUSMA) kilitangaza kuhitimisha rasmi majukumu yake nchini humo baada ya kuhudumu kwa muda wa miaka kumi.
Kuondoka kwa kikosi cha MINUSMA ni sehemu ya kurekebisha upya mpango wa usalama ulioanzishwa na utawala wa kijeshi wa Mali uliochukua mamlaka mwaka 2020.