Somalia kusimamisha safari za shirika la ndege la Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115532-somalia_kusimamisha_safari_za_shirika_la_ndege_la_ethiopia
Mamlaka ya usafiri wa anga nchini Somalia imetishia kusitisha safari zote za ndege za Shirika la ndege la Ethiopia (Ethiopia Airlines) kwenda nchini humo, hatua ambayo itazidi kuzorotesha uhusiano dhaifu kati ya nchi hizo jirani.
(last modified 2026-05-13T18:57:29+00:00 )
Aug 22, 2024 23:26 UTC
  • Somalia kusimamisha safari za shirika la ndege la Ethiopia

Mamlaka ya usafiri wa anga nchini Somalia imetishia kusitisha safari zote za ndege za Shirika la ndege la Ethiopia (Ethiopia Airlines) kwenda nchini humo, hatua ambayo itazidi kuzorotesha uhusiano dhaifu kati ya nchi hizo jirani.

Mamlaka hiyo ya usafiri wa anga ya Somalia SCAA imesema shirika la ndege la Ethiopia Airlines, ambalo ni shirika kubwa zaidi la ndege barani Afrika, halijashughulikia malalamiko ya hapo awali ikiwemo kile walichokiita “masuala ya uhuru.”

Mamlaka hiyo imeeleza kuwa, iwapo malalamiko hayo hayatapa ufumbuzi kufikia leo Agosti 23, basi haitakuwa na budi ila kusimamisha safari zote za ndege za Ethiopian Airlines kwenda Somalia.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Somalia na Ethiopia, zipo kwenye mvutano wa kidiplomasia baada ya Addis Ababa kuingia kwenye makubaliano na jimbo la Somaliland la Somalia mapema mwaka huu ambalo limeipa Ethiopia eneo la bahari lenye urefu wa Kilomita 20.

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud

 

Hii inakuja pia siku chache baada ya rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud Jumamosi iliyopita kuishtumu Ethiopia kwa kutoikubali nchi yake kuwa ina mamlaka ya huru na kujitegemea, huku mazungumzo ya hivi karibuni kati ya nchi hizo mbili yaliyofanyika nchini Uturuki yakifikia tamati bila natija ya kuridhisha.

Shirika la ndege la Ethiopia lina safari za ndege zinazokwenda kwenye mji mkuu wa Somaliland Hargeisa, pamoja na mji mkuu wa Somalia Mogadishu na miji minne ya majimbo ya Somalia.