Watu milioni 63 hawana chakula cha uhakika Pembe ya Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115538-watu_milioni_63_hawana_chakula_cha_uhakika_pembe_ya_afrika
Takriban watu milioni 63 katika eneo la Pembe ya Afrika wana uhaba mkubwa wa chakula huku watoto milioni 11 wakiwa na utapiamlo na wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.
(last modified 2024-08-23T03:01:42+00:00 )
Aug 23, 2024 03:01 UTC
  • Watu milioni 63 hawana chakula cha uhakika Pembe ya Afrika

Takriban watu milioni 63 katika eneo la Pembe ya Afrika wana uhaba mkubwa wa chakula huku watoto milioni 11 wakiwa na utapiamlo na wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.

Hayo yamo kwenye ripoti ya jana Alkhamisi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD) iliyotolewa jijini Nairobi Kenya ambayo imesema, migogoro, mabadiliko ya hali ya hewa, mfumuko wa bei na madeni makubwa yamezidisha njaa na utapiamlo kwa wakazi wa nchi za eneo hilo.

Katibu Mtendaji wa IGAD, Workneh Gebeyehu amesema wakati wa uzinduzi wa mtandaoni wa ripoti hiyo kwamba: "Takwimu hizi zinaonyesha kuweko mgogoro wa kibinadamu katika eneo letu ambapo hali mbaya ya hewa na mtikisiko wa kiuchumi unasababisha viwango vya juu vya uhaba wa chakula na hivyo kuyatumbukiza hatarini maisha ya mamilioni ya watu."

Gebeyehu amezitaka nchi saba wanachama wa IGAD ambazo ni Djibouti, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Uganda kuimarisha jumuiya za ndani zinazokabiliana na uhaba wa chakula na maji unaosababishwa na hali ya hewa.

Athari zinazoendelea za janga la UVIKO-19, misimu mitano mfululizo wa ya uhaba wa mvua, mafuriko yanayohusiana na El-Nino na mapigano na mizozo ya ndani imeongeza mgogoro wa njaa katika eneo kubwa la Pembe ya Afrika.