Watu 26 wateketea kwa moto katika ajali mbaya ya barabarani nchini Malawi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115540-watu_26_wateketea_kwa_moto_katika_ajali_mbaya_ya_barabarani_nchini_malawi
Takriban watu 26 wameteketea kwa moto hadi kufa nchini Malawi kufuatia kuwaka moto gari moja dogo baada ya kugonga lori la mafuta.
(last modified 2024-08-23T03:04:00+00:00 )
Aug 23, 2024 03:04 UTC
  • Watu 26 wateketea kwa moto katika ajali mbaya ya barabarani nchini Malawi

Takriban watu 26 wameteketea kwa moto hadi kufa nchini Malawi kufuatia kuwaka moto gari moja dogo baada ya kugonga lori la mafuta.

Shirika la habari la Anadolu limemnukuu Harry Namwaza, naibu msemaji wa Huduma ya Polisi ya Malawi, akisema baada ya ajali hiyo ya Jumatano iliyotoka katika wilaya ya Kasungu ya Kati kwamba: "Abiria wote waliokuwemo kwenye gari dogo "wameteketea kikamilifu kwa moto na hakuna hata mmoja aliyenusurika na kutoka salama."

Amesema: “Dereva wa gari la abiria alikuwa katika mwendo kasi na aliishia kuligonga lori la mafuta wakati alipokuwa anajaribu kulipita kwa kasi kubwa.” 

Ameongeza kwamba, gari hilo la abiria lilikuwa njiani kuelekea mji mkuu wa nchi hiyo, Lilongwe.

Ajali za barabarani hugharimu maisha ya watu wengi kila wiki katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

Kwa mujibu wa ripoti ya Huduma ya Polisi ya Malawi, nchi hiyo ilirekodi ajali 4,977 mwaka jana, zikiwemo 389 ambazo zilisababisha vifo.

Wiki iliyopita, takriban watu 10 waliripotiwa kufariki dunia baada ya gari lililokuwa likiendeshwa kwa kasi kuvamia soko kusini mwa nchi hiyo.

Viongozi wa Serikali ya Malawi, wahandisi wa barabara na wataalamu wa usalama barabarani wanazihusisha ajali hizo na tabia mbaya za madereva na ubovu wa barabara.