Zaidi ya watu milioni 25 wamekimbia makazi yao katika Pembe ya Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115568-zaidi_ya_watu_milioni_25_wamekimbia_makazi_yao_katika_pembe_ya_afrika
Takriban watu milioni 25 walikuwa wakimbizi wa ndani katika eneo la Pembe ya Afrika mwishoni mwa Juni, ikiwa ni pamoja na wakimbizi milioni 20 wa ndani katika nchi sita na wakimbizi milioni 5 waliokimbilia nje ya nchi hizo.
(last modified 2026-05-13T18:57:29+00:00 )
Aug 23, 2024 23:04 UTC
  • Zaidi ya watu milioni 25 wamekimbia makazi yao katika Pembe ya Afrika

Takriban watu milioni 25 walikuwa wakimbizi wa ndani katika eneo la Pembe ya Afrika mwishoni mwa Juni, ikiwa ni pamoja na wakimbizi milioni 20 wa ndani katika nchi sita na wakimbizi milioni 5 waliokimbilia nje ya nchi hizo.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD) na Shiŕika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) kanda ya Afrika Mashariki, eneo hilo bado lina idadi kubwa zaidi ya watu waliokimbia makazi yao kwa nguvu duniani.

Taasisi hizo mbili zimesema: "Mgogoro nchini Sudan umesababisha ongezeko la kutisha la idadi ya wakimbizi wa kikanda tangu mwishoni mwa mwaka 2023, kutoka milioni 20.5 hadi milioni 25 kufikia katikati ya mwaka 2024."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, viwango vya juu vya uhaba wa chakula na utapiamlo vimeenea miongoni mwa watu waliokimbia makazi yao katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa IGAD na IOM, zaidi ya nusu ya wakimbizi milioni 20 wa ukanda huo wako Sudan, wakifuatiwa na Somalia na Ethiopia.

Tangu vilipoanza vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi huko Sudan mwezi Aprili 2023 hadi hivi sasa, watu milioni 7.9 wameshakimbia makazi yao na mgogoro huu kuufanya kuwa mkubwa zaidi wa wakimbizi wa ndani duniani.

Takriban watu milioni 2.3 wamekimbilia nchi jirani, huku thuluthi nzima kati yao wakiwa wamekimbilia katika nchi jirani ya Sudan Kusini.