Almasi kubwa zaidi katika karne yapatikana nchini Botswana
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115578-almasi_kubwa_zaidi_katika_karne_yapatikana_nchini_botswana
Almasi kubwa zaidi iliyowahi kupatikana  katika zaidi ya karne moja imechimbuliwa katika mgodi mmoja nchini Botswana, na rais wa nchi hiyo aliuonyesha ulimwengu jiwe hilo lenye ukubwa wa ngumi katika hafla ya kulitazama.
(last modified 2024-08-24T03:13:52+00:00 )
Aug 24, 2024 03:13 UTC
  • Almasi kubwa zaidi katika karne yapatikana nchini Botswana

Almasi kubwa zaidi iliyowahi kupatikana  katika zaidi ya karne moja imechimbuliwa katika mgodi mmoja nchini Botswana, na rais wa nchi hiyo aliuonyesha ulimwengu jiwe hilo lenye ukubwa wa ngumi katika hafla ya kulitazama.

Rais wa Botswana Mokgweetsi Masisi alisema. "Almasi inamaanisha kila kitu kwetu katika nyakati nzuri na wakati wa maafa."

Serikali ya Botswana inasema almasi hiyo kubwa ya karati 2,492 ni ya pili kwa ukubwa kuwahi kugunduliwa katika mgodi. Ni almasi kubwa zaidi kupatikana tangu ile iliyopatikana Afrika Kusini mwaka 1905.

Maafisa wamesema ni mapema mno kuthamini jiwe hilo au kuamua jinsi litakavyouzwa. Almasi nyingine ndogo kutoka mgodi huo nchini Botswana iliuzwa kwa dola milioni 63 mwaka 2016.

Naseem Lahri, mkurugenzi mtendaji wa Botswana wa Lucara Diamond Corp, kampuni ya uchimbaji madini ya Kanada iliyopata almasi hiyo anasema kuwa almasi hii imepatikana kutokana na teknolojia iliyotumika ambayo ni ya  XRT.

Alisema katika taarifa yake Jumatano kwamba walipata almasi hii "ya kipekee" kutoka Mgodi wa Karowe katikati mwa Botswana.

Botswana, nchi yenye watu milioni 2.6 kusini mwa Afrika, ni ya pili kwa ukubwa wa almasi ya asili nyuma ya Russia na imefukua mawe yote makubwa zaidi duniani katika miaka ya hivi karibuni. Pamoja na hayo wananchi wa Botswana wamekuwa wakilalamika kuwa wanadhulumiwa na makampuni makubwa ya uchimbaji madini. Rais Masisi pia amekuwa akitaka mashirika ya madini yaipe nchi hiyo hisa zaidi katika faida zinazotokana na madini.