Wanafunzi wa vyuo vikuu waliokuwa wametekwa nyara Nigeria waachiliwa huru
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115608-wanafunzi_wa_vyuo_vikuu_waliokuwa_wametekwa_nyara_nigeria_waachiliwa_huru
Polisi nchini Nigeria wametangaza kuachiliwa huru wanafunzi 20 wa taaluma ya tiba waliotekwa nyara Agosti 15 katika jimbo la kati la Benue.
(last modified 2024-08-25T00:23:41+00:00 )
Aug 25, 2024 00:23 UTC
  • Wanafunzi wa vyuo vikuu waliokuwa wametekwa nyara Nigeria waachiliwa huru

Polisi nchini Nigeria wametangaza kuachiliwa huru wanafunzi 20 wa taaluma ya tiba waliotekwa nyara Agosti 15 katika jimbo la kati la Benue.

Msemaji wa polisi Olumuyiwa Adejobi ameziambia duru za habari kwamab, wanafunzi hao waliokolewa kupitia juhudi za pamoja za vyombo vya usalama, wenyeji na ofisi ya mshauri wa usalama wa taifa.

Wanafunzi kutoka vyuo vikuu vya Maiduguri na Jos walitekwa nyara walipokuwa wakisafiri kwenda kwenye kongamano la kila mwaka kusini mashariki mwa jimbo la Enugu.

Mkuu wa polisi nchini Nigeria Kayode Egbetokun aliimarisha msako huo wiki iliyopita kwa kuagiza timu maalum za polisi kutumia helikopta, ndege zisizo na rubani na magari maalumu kuwaokoa wanafunzi hao.

Watekaji nyara hao walikuwa wametishia kuanza kuwaua baadhi ya wanafunzi hao iwapo hawatapata fedha hizo, kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo. Bw Olumuyiwa alisema kuwa waliachiliwa "bila ya fidia yoyote kulipwa.

Aprili mwaka huu (2024) ilitimia miaka kumi tangu kundi la Boko Haram nchini Nigeria liishambulie shule ya sekondari ya wanafunzi wa kike katika jimbo la Borno katika jamii ya Chibok na kuwateka nyara karibu mabinti 300.

 

Kundi la kigaidi la Boko Haram na makundi mengine ya wabeba silaha yamekuwa yakijihusisha na utekaji nyara wanafunzi nchini Nigeria na kudai kikomboleo. Hadi sasa wanafunzi wasiopungua 1500 wametekwa nyara huko Nigeria tangu mwaka 2014; huku makundi yenye silaha yakistafidi na mbinu hiyo ya utekaji nyara kama njia ya kupata fedha kwa ajili ya kufadhili jinai zao nyingine na kudhibiti vijiji katika maeneo tajiri kwa madini ya kaskazini magharibi mwa Nigeria hata hivyo yenye ulinzi dhaifu wa polisi.