Uganda yaripoti maambuziko mengine ya homa ya Mpox
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115614-uganda_yaripoti_maambuziko_mengine_ya_homa_ya_mpox
Wizara ya Afya ya Uganda imetangaza kuwa, visa vingine viwili vya virusi vya homa ya Mpox vimethibitishwa nchini humo na kuongeza idadi ya walioambukizwa kuwa watu wanne, katika taifa hilo la Afrika Mashariki.
(last modified 2024-08-25T03:45:42+00:00 )
Aug 25, 2024 03:45 UTC
  • Uganda yaripoti maambuziko mengine ya homa ya Mpox

Wizara ya Afya ya Uganda imetangaza kuwa, visa vingine viwili vya virusi vya homa ya Mpox vimethibitishwa nchini humo na kuongeza idadi ya walioambukizwa kuwa watu wanne, katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Mkuregenzi Mkuu wa Huduma ya Afya nchini Uganda, Henry Mwebesa, ameziambia duru za habari kwamba, wagonjwa hao wawili wapya wanasemekana kuambukizwa kirusi cha Clade b1.

Wagonjwa hao ambao mmoja ni dereva wa lori, kwa sasa wamewekwa karantini katika hospitali moja iliyoko Entebbe.

Uganda iliripoti kisa cha kwanza Julai 24 wakati vipimo vya maabara vya wagonjwa wawili katika hospitali moja inayopakana na Jamhuri ya kidemkrasia ya Kongo, vilipogundua kuambukizwa homa hiyo.

Wiki iliyopita, Shirika la Afya Duniani (WHO) liliitangaza Mpox kuwa "dharura ya afya ya umma" kwa mara ya pili sasa katika kipindi cha miaka miwili.

Kabla ya hapo pia, Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika, CDC, kilitangaza "dharura ya afya ya umma", kiwango chake cha juu zaidi cha tahadhari, juu ya mripuko wa Mpox unaoenea kwa kasi katika bara hilo, na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za kukomesha kusambaa kwake.

Jumla ya visa 38,465 vya ugonjwa huo, ambao zamani ulijulikana kama homa ya nyani, vimerekodiwa katika nchi 16 za Afrika tangu mwezi Januari 2022, pamoja na vifo 1,456, na ongezeko la 160% la kesi mwaka huu 2024 ikilinganishwa na mwaka uliopita, kulingana na data zilizochapishwa wiki iliyopita na Africa CDC.

Kesi za Mpox ziliripotiwa kwa mara ya kwanza wiki iliyopita katika nchi za Burundi na Rwanda baada ya kuripoti mripuko wa maradhi hayo DRC; huku kesi zaidi zikigunduliwa nchini Kenya na Jamhuri ya Afrika ya Kati.