Magaidi 19 wa al-Shabaab wauawa katika mashambulizi ya anga Somalia
Wanachama wasiopungua 19 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab wameuawa katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa na jeshi la Somalia katika maeneo ya Shabelle ya Kati na Galgadud.
Operesheni hizo za anga dhidi ya kundi hilo la kigaidi lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda zilidumu kwa zaidi ya saa 24 katika vijiji vya Run-Nirgod, Masagaway na El-Dher. Shirika la habari la Anadolu limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, magari yaliyokuwa yanatumiwa na magaidi hao pia yaliharibiwa.
Wizara ya Habari ya Somalia imesema katika taarifa kuwa, "Operesheni ya kwanza iliyodumu kwa zaidi ya saa 24 ilifanyika katika kijiji cha Geed Ma'arke wilayani Ruunirgood, ambapo 'Khawaarij' walikuwa wakijitayarisha (kufanya hujuma) ambapo zaidi ya magaidi 14 wameuawa."
Operesheni ya pili, kwa mujibu wa wizara hiyo, ililenga kituo cha upekuzi cha magaidi, ambapo wanamgambo wasiopungua watano wameangamizwa. Operesheni nyingine ililenga kambi ya magaidi, ambayo pia iliharibu magari ya kijeshi.

Ikumbukwe kuwa, Agosti 3, watu wapatao 37 waliuawa katika shambulio la bunduki linaloaminika kutekelezwa na wanamgambo hao wa al-Shabaab kwenye ufukwe maarufu katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi la al-Shabaab limekuwa likipambana na serikali ya Somalia na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika. Al-Shabaab imeongeza mashambulizi tangu Rais Hassan Sheikh Mohamud alipotangaza kuanzishwa "vita kamili vya pande zote" dhidi ya kundi hilo la kigaidi.