Jul 20, 2016 07:31 UTC
  • 39 wauawa na kujeruhiwa katika hujuma dhidi ya kambi ya jeshi Mali

Askari 12 wa jeshi la Mali wameuawa katika shambulizi lililotekelezwa na waasi mapema jana katikati mwa nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika.

Ousmane Diallo, Naibu wa Meya wa mji unaopakana na eneo la Nampala amethibitisha kutokea uvamizi huo na kuongeza kuwa, raia 27 wamejeruhiwa katika shambulizi hilo dhidi ya kambi ya jeshi ya Nampala, katika mpaka wa nchi hiyo na Mauritania. Aidha duru za kiusalama zimeripoti kuwa, wavamizi waliotekeleza hujuma hiyo kwa sasa wanaidhibiti kambi hiyo ya jeshi. Kwa mujibu wa duru za jeshi nchini Mali, shambulizi hilo limesababisha uharibifu mkubwa mbali na vifo hivyo. Inafaa kufahamika kuwa, Mali imekuwa ikikumbwa na mashambulizi ya makundi ya wabeba silaha katika maeneo ya kaskazini, tangu taifa hilo lilipokumbwa na mapigano ya mwaka 2012 na sasa maeneo ya katikati mwa nchi hiyo yamegeuka na kuwa uwanja wa machafuko. Licha ya kuwepo askari wa Ufaransa na askari wa Umoja wa Mataifa nchini humo, lakini makundi ya wabeba silaha na yale yenye siasa kali, yameendeleza harakati zao.

Tags