Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Misri na Sudan wakutana kujadili vita vya Sudan
(last modified Tue, 10 Sep 2024 11:14:51 GMT )
Sep 10, 2024 11:14 UTC
  • Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Misri na Sudan wakutana kujadili vita vya Sudan

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty, amekutana na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Sudan, Hussein Awad, na kujadiliana naye juhudi za kutatua mgogoro wa nchi hiyo.

Hayo yametangazwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri ambayo imeongeza kuwa, katika mazungumzo hayo, Badr Abdelatty amesema kuwa Misri imejitolea kupigania umoja, haki ya kujitawala na uadilifu katika maeneo yote ya Sudan.

Taarifa hiyo vilevile imesema: Abdelatty ametilia mkazo pia juhudi za Cairo za kuwaunga mkono raia wa Sudan wanaoishi Misri, na kuwahakikishia usalama wao hadi waweze kurejea kwao nchini Sudan.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan ameishukuru Misri kwa mchango wake katika kuutafutia suluhu mgogoro wa ndani wa Sudan.

Tangu Aprili 15, 2023, Sudan imetumbukia kwenye mgogoro mkubwa wa vita vya uchu wa madaraka kati ya Jeshi la Sudan SAF na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 16,650.

Takwimu za karibuni kabisa zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zinasema kwamba, karibu watu milioni 10.7 wamekimbia makazi yao ndani ya Sudan, huku takriban milioni 2.2 wakitafuta hifadhi katika nchi jirani hasa Sudan Kusini. Nchi nyingine zenye wakimbizi wengi wa Sudan ni Chad na Misri.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi zilizotolewa mwezi Machi na serikali ya Misri, takriban Wasudan 500,000 wamekimbilia Misri tangu ulipoanza mgogoro huo wa uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi wa Sudan.