Somalia yakumbwa na mlipuko karibu na ikulu ya Rais, watu kadhaa wauawa
Watu kadhaa wanahofiwa kuuawa au kujeruhiwa baada ya mlipuko mkubwa kutokea leo katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Afisa mmoja wa usalama wa Somalia ameeleza kuwa, mlipuko huo unaaminika kuwa ni umesabishwa na mlipuko wa bomu la kujitoa mhanga uliokusudiwa mgahawa mmoja uliokuwa na wateja watu wengi karibu na makumbusho ya taifa.
Hadi sasa idadi kamili ya waliopoteza maisha katika mlipuko huo haijatangazwa.
Eneo hilo la mgahawa karibu na Makumbusho ya Taifa mjini Mogadishu linajulikana kwa kutembelewa na maafisa wa ngazi ya juu wa serikali wakiwemo maafisa usalama wa Somalia huku Ikulu ya Rais pia ikiwa karibu na eneo hilo.
Hadi sasa hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo. Kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na al-Qaed limekuwa likitekeleza mashambulizi kama hayo huko Somalia likiwemo moja katika wiki za hivi karibuni.
