Jeshi la Nigeria laua 'magaidi' 187 ndani ya wiki moja
Zaidi ya watu 187 wanaoshukiwa kuwa magaidi wameuawa huku wengine 262 wakikamatwa katika operesheni mbalimbali za kupambana na ugaidi za jeshi la Nigeria nchini kote katika muda wa wiki moja iliyopita.
Shirika la habari la Xinhua la China limemnukuu Edward Buba, Msemaji wa Jeshi la Nigeria akisema hayo katika taarifa ya jana Jumamosi katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja.
Buba ameeleza kuwa, watu 19 wanaoshukiwa kuwa magaidi wamejisalimisha kwa wanajeshi wa nchi hiyo kati ya Oktoba 23 na 29 wakati wa operesheni hizo za kutokomeza ugaidi.
Amesema kuwa, jeshi limepata "mafanikio makubwa" katika operesheni zake hizo za kupambana na ugaidi, akibainisha kuwa Abubakar Ibrahim, mshukiwa maarufu wa ugaidi anayejulikana pia kama Habu Dogo, alikamatwa katika kijiji kimoja kaskazini magharibi mwa jimbo la Sokoto katika kipindi hicho.
Habu Dogo, mmoja wa vinara "wanaosakwa zaidi" nchini humo, amekuwa kwenye orodha ya vyombo vya usalama vya Nigeria na nchi jirani ya Niger kutokana na "kuchupa mpaka kwenye shughuli zake za kigaidi," msemaji huyo wa jeshi ameongeza.
Haya yanaripoti katika hali ambayo, juzi Ijumaa, watu 15 waliuawa katika shambulizi la 'magaidi' waliojizatiti kwa silaha katika jimbo la Benue katikati mwa Nigeria.