Somalia yasema Ethiopia haitaruhusiwa kuchangia askari wa kikosi kipya cha AU
Somalia imesisitiza kwamba Ethiopia haitakuwa sehemu ya ujumbe mpya wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika nchini humo, huku mataifa hayo mawili yakisalia katika mzozo ambao umesababisha mtikisiko katika Pembe ya Afrika.
Wanajeshi wa Umoja wa Afrika wamekuwa wakishiriki katika mapambano dhidi ya magaidi wa Al-Shabaab nchini Somalia tangu mwaka 2007, kwa lengo la kukabidhi jukumu la usalama kwa vikosi vya jeshi la taifa.
Kikosi cha sasa cha AU nchini Somalia kinachojulikana kama ATMIS - ambacho kinajumuisha takriban wanajeshi 3,000 wa Ethiopia - kinatarajiwa kumalizia shughuli zake rasmi mwishoni mwa mwaka huu, na nafasi yake kuchukuliwa na kikosi kilichoboreshwa kiitwacho AUSSOM.
Waziri wa Ulinzi wa Somalia, Abdulkadir Mohamed Nur, amesema katika mahojiano ya televisheni kwamba Ethiopia ndiyo serikali pekee tunayoifahamu hadi sasa ambayo haitachangia askari katika kikosi kipya kwa sababu imekiuka mamlaka na umoja wetu.
Majirani hao wawili wamekuwa katika mzozo tangu Ethiopia isiyo na bandari mwezi Januari ilipofikia makubaliano na eneo la Somalia lililojitenga linajulikana kama Somaliland ambapo itakodisha eneo la pwani kwa ajili ya bandari na kambi ya kijeshi.
Mogadishu, ambayo haijawahi kutambua tangazo la uhuru la Somaliland mwaka 1991, imeyataja makubaliano hayo kuwa ni shambulio dhidi ya mamlaka yake.
Pamoja na Ethiopia, ambayo pia ina wanajeshi nchini Somalia wanaofanya kazi chini ya mikataba tofauti ya nchi mbili, nchi nyingine zinazochangia kikosi cha AU ni pamoja na Burundi, Djibouti, Kenya na Uganda.
Nur amesema Somalia itazindua utaratibu wa kualika serikali kushiriki katika kikosi cha AUSSOM, ambacho kinatarajiwa kufanya kazi hadi mwisho wa 2028.