Wananchi wa Gabon wapasisha katiba mpya kupitia kura ya maoni
(last modified Tue, 19 Nov 2024 02:41:09 GMT )
Nov 19, 2024 02:41 UTC
  • Wananchi wa Gabon wapasisha katiba mpya kupitia kura ya maoni

Wananchi wa Gabon wamepasisha katiba mpya ya nchi hiyo kwa wingi wa kura katika zoezi la kura ya maoni lililofanyika Jumamosi iliyopita.

Kulingana na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Gabon Hermann Immongault, 91.80% ya wapiga kura walipigia kura ya "ndio" Katiba mpya, dhidi ya 8.20% ya "Hapana", Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Gabon, kiwango cha ushiriki katika kura hiyo ya maoni kilifikia 53.54%.

Katiba mpya Gabon inampa mamlaka makubwa zaidi Rais. Aidha kwa mujibu wa katiba mpya, Rais ataongoza kwa mihula miwili ya miaka saba saba badala ya miaka mitano mitano ya awali. Kadhalika Rais wa Jamhuri atakuwa mkuu wa serikali kwa kuwa nafasi ya Waziri Mkuu itafutwa. Pia ataweza kulivunja Bunge angalau mara moja wakati wa muhula wake, wakati Bunge linaweza kumfungulia mashtaka katika Mahakama Kuu ya Haki.

Rais wa mpito Brice Oligui Nguema alichukua mamlaka katika mapinduzi ya mwaka jana, na kumuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu Ali Bongo ambaye alikuwa ameshinda uchaguzi wa marudio.

Uchaguzi umepangwa kufanyika Agosti 2025, na Jenerali Nguema anaweza kugombea, kulingana na baadhi ya wachambuzi wa kisiasa. Katiba mpya ikipitishwa itampa mamlaka ya kushindana.

Wanaounga mkono katiba inayopendekezwa wanasema, rasimu ya hiyo ya sheria inawakilisha kujiondoa kwenye utawala wa miaka 55 wa familia ya Bongo.

Lakini wakosoaji wanasema inaweza kumpatia rais madaraka makubwa zaidi, na wanahofia hatua hiyo inaweza kumuingiza madarakani mtawala mpya.