Utawala wa kijeshi Mali wamteua waziri mkuu mpya baada ya kumtimua Maiga
Baraza la utawala wa kijeshi la Mali jana Alkhamisi lilimteua msemaji wake, Abdoulaye Maiga, kuwa waziri mkuu siku moja baada ya kumfukuza kazi Choguel Maiga ambaye alikosoa utawala huo kwa kuahirisha uchaguzi wa kidemokrasia na kurejesha utaratibu wa Katiba.
Choguel Maiga alinukuliwa mwishoni mwa wiki akikosoa kushindwa kwa utawala wa kijeshi wa Mali kuandaa uchaguzi ndani ya kipindi cha mpito kilichoahidiwa cha miezi 24 kwa ajili ya kurejesha utawala wa kidemokrasia, kauli ambayo iliwakasirisha majenerali wanaotawala.
Watawala wa kijeshi, waliochukua mamlaka katika mapinduzi ya mwaka wa 2020 na 2021, walikuwa wameahidi kufanya uchaguzi mwezi Februari lakini wameahirisha zoezi hilo kwa muda usiojulikana kutokana na masuala ya kiufundi.
Mwishoni mwa mwaka jana jeshi la Mali lilitangaza kwamba litaahirisha uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika Februari ambao unanuia kurejesha mamlaka ya kiraia madarakani.
Sababu zilizotolewa na afisa mmoja wa jeshi hilo ni pamoja na masuala yanayohusiana na kupitishwa kwa katiba mpya mwaka huu na mapitio ya orodha za wapiga kura. Rais wa Mali anachaguliwa kwa muhula wa miaka mitano.