Ramaphosa: G-20 ijihadhari na sera za Trump za "Marekani Kwanza"
Wakati dunia ikisubiri kuapishwa rais mteule wa Marekani, Donald Trump, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametahadharisha kuhusu sera za kiongozi huyo mpya za "Marekani Kwanza".
Ramaphosa amewahakikishia wakuu wa kundi la G-20 kuhusu hatua husika ambazo wamechukua za kujihadhari na sera ya Trump ya "Marekani Kwanza" katika muhula wake wa pili wa uongozi utakaoanza Januari 20.
"Nadhani kutakuwa na hatua za kutosha ambazo zitaliwezesha G20 kuendelea kufanya kazi kwa njia ambayo itaendeleza maslahi ya ulimwengu, na kumbuka pia kuwa, kupitia G20 hatupigi hatua kwa ajili ya maslahi ya nchi moja tu, bali tunaendeleza maslahi ya watu wa dunia nzima,” amesema Rais wa Afrika Kusini.
Trump amedokeza kuwa sera zake za nje zitakuwa za makabiliano. Ameahidi kuweka ushuru mpya dhidi ya China, Mexico na Canada huku akitishia kuziwekea ushuru wa asilimia 100 nchi wanachama wa BRICS zinazozijumuisha Brazil, Russia, China, India, Afrika Kusini na nyinginezo iwapo zitazindua sarafu yao makhsusi.

Donald Trump aliandika katika ukurasa wake wa X kwamba nchi hizo zote zinapasa kutazamia kuagana na kile alichokiita kuwa "biashara ya aina yake ya uchumi wa Marekani" iwapo zitaendelea kujikita na sera ya kuacha kutegemea sarafu dola ya Marekani katika biashara ya kimataifa.