Jumuiya ya SADC yakabidhiwa rasmi jengo jipya la Makao Makuu yake nchini Botswana
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120150-jumuiya_ya_sadc_yakabidhiwa_rasmi_jengo_jipya_la_makao_makuu_yake_nchini_botswana
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ambaye ndiye mwenyekiti wa hivi sasa wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Rais Duma Boko wa Botswana wamewawakilisha viongozi wengine wa jumuiya na kupokea rasmi jengo la Makao Makuu ya SADC huko Gaborone, mji mkuu wa Botswana.
(last modified 2024-12-14T23:35:34+00:00 )
Dec 14, 2024 23:35 UTC
  • Jumuiya ya SADC yakabidhiwa rasmi jengo jipya la Makao Makuu yake nchini Botswana

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ambaye ndiye mwenyekiti wa hivi sasa wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Rais Duma Boko wa Botswana wamewawakilisha viongozi wengine wa jumuiya na kupokea rasmi jengo la Makao Makuu ya SADC huko Gaborone, mji mkuu wa Botswana.

Serikali ya Botswana imetoa taarifa rasmi na kusema kuwa, jengo hilo limesanifiwa, kujengwa na kusimamiwa chini ya makubaliano ya ushirikiano wa sekta za umma na sekta binafsi kati ya SADC, shirika la Bongwe Investments Proprietary Limited na serikali ya Botswana.

Wakati wa hafla ya kukabidhiana ofisi hiyo, Mnangagwa amesema kuwa, jengo hilo linaashiria ushirikiano mzuri na umoja kati ya nchi wanachama wa SADC.

Amesema: "Nyumba ya SADC inasimama kama ishara kuu ya mshikamano, umoja, uhuru na kujitegemea... lakini muhimu zaidi, inatuleta pamoja kama kanda."

Aliipongeza Botswana kwa kugharamia fedha za kujengea Sekretarieti ya SADC na kusisitiza kuwa, mazingira mazuri yataiwezesha sekretarieti hiyo kutekeleza vyema majukumu yake.

Kwa upande wake Rais Boko ametilia mkazo dhamira ya Botswana ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda wa SADC na bara la Afrika kwa ujumla, akiongeza kuwa, uamuzi wa nchi yake wa kuipa ardhi SADC kwa ajili ya kuendeshea shughuli zake unaonesha dhamira ya nchi za jumuiya hiyo katika kuimarisha amani na usalama wa eneo hilo lote.