Rais Pezeshkian ampongeza Papa Leo, asema Iran bado imejitolea kwa diplomasia
-
Rais Pezeshkian amepongeza misimamo ya Papa Leo dhidi ya sera za vita za Marekani, Israel
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepongeza misimamo ya kimaadili ya Papa Leo XIV kuhusu uchokozi wa hivi karibuni wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran, akisisitiza haja ya jamii ya kimataifa kuchukua mwelekeo unaotilia maanani hali halisi na wa haki, na kutoa wito kwa nchi zote duniani kukabiliana na matakwa haramu na sera za kibabe na hatari za Marekani.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, leo Jumamosi ameandika katika ujumbe uliotumwa kwa kiongozi wa Wakatoliki duniani Papa Leo XIV akisema: "Mbinu ya uharibifu ya Marekani na utawala wa Israel na mashambulizi yao haramu si dhidi ya Iran pekee, bali pia dhidi ya utawala wa sheria katika ngazi ya kimataifa, sheria za kimataifa, maadili ya binadamu na mafundisho ya dini za Mungu. Ni wazi kwamba gharama za mbinu hii hatari zitabebwa na jamii nzima ya kimataifa."
Rais Pezeshkian amesisitiza kwamba Iran imethibitisha mara kwa mara kufungamana kwake na diplomasia na suluhisho la amani kwa ajili ya kutatua masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mzozo wake na serikali ya Marekani.
Amesema kwamba licha ya usaliti wa mara kwa mara wa Marekani kwenye meza ya mazungumzo, Iran imekaribisha upatanishi wa Pakistan na kuingia katika mazungumzo ya Islamabad kwa nia njema na kitaaluma.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amenukuu matamshi hatari na yasiyo na aibu ya Rais wa Marekani, Donald Trump kuhusu nia ya "kuharibu ustaarabu wa kihistoria wa Iran na kuurudisha kwenye Enzi ya Mawe."
Amesema matamshi haya "yanatokana na njozi za kuwa na nguvu mutlaki na yana mizizi katika kiburi, uonevu, uchoyo, na jaribio la kusuluhisha migogoro kupitia mabavu; jambo ambalo dhamiri ya mwanadamu haiwezi kulielewa au kulivumilia."
Rais Pezeshkian amesema kwamba utumiaji wa kambi za kijeshi za Marekani katika nchi za Ghuba ya Uajemi kwa ajili ya mashambulizi dhidi ya Iran ulivilazimisha Vikosi vya Jeshi vya Iran kulenga maslahi na mali za wavamizi katika nchi hizo kwa ajili ya kujilinda.
Rais Masoud Pezeshkian amemalizia kwa kuthibitisha tena kujitolea Iran kwa ajili ya mazungumzo na utatuzi wa matatizo kwa amani, akisema kwamba mapambano ya Iran dhidi ya matakwa haramu ya Marekani ni sawa na kutetea sheria za kimataifa na maadili ya kibinadamu.