Mwendesha Mashtaka wa Umma Sudan aahidi kuwafungulia mashtaki makamanda wa RSF
-
Al-Fatih Mohamed Issa Tayfour
Mwendesha Mashtaka wa Umma nchini Sudan, Al-Fatih Mohamed Issa Tayfour, ameahidi kuwafungulia mashtaka wanamgambo wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) katika mahakama za kitaifa.
Mohamed Issa Tayfour, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Uhalifu na Ukiukaji wa Sheria za Kitaifa na Sheria za Kibinadamu za Kimataifa, amesema kuwa Vikosi vya Msaada wa Haraka "vimefanya uhalifu wa kutisha ambao unaaibisha ubinadamu, haswa uhalifu wa mauaji ya kimbari dhidi ya Watu wa Masalit katika mji wa El Geneina katika jimbo la Darfur Kaskazini, pamoja na kuwashambulia raia kwa kuwaua wanaume na kuwabaka wanawake."
Issa Tayfour, amesema katika taarifa yake iliyochapishwa jana, Jumatatu huko Port Sudan kwamba serikali ya Sudan itawafungulia mashtaka wapiganaji wa RSF mbele ya mahakama za kitaifa, na amepongeza ufanisi wa mahakama ya kitaifa na taasisi za mahakama, akisema, "Tuna mahakama yenye historia ndefu na ya haki na uendesha mashtaka ya umma wenye uwezo wa kutimiza majukumu yote uliyopewa."
Mwendesha Mashtaka wa Umma wa Sudan amefichua kuwa kumefanyika mawasiliano na baadhi ya nchi kuhusiana na kurejeshwa nchini washtakiwa hao, akisisitiza kuwa wasiporejeshwa, taratibu zitaendelea na watafunguliwa mashtaka bila kuwepo mahakamani.
Al-Fatih Mohamed Issa Tayfour amegusia uhalifu na ukiukaji wa sheria za kitaifa na za kimataifa uliofanywa na wapiganaji wa RSF katika Jimbo la Jazira, kama mauaji, ubakaji, kuwafukuza watu kwenye makazi yao na uhalifu mwingine unaofanywa na wapiganaji wa kundi hilo.
Tangu katikati ya Aprili 2023, jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka vimekuwa vikipigana vita ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya wa 20,000. Zaidi ya Wasudani milioni 14 pia wamelazimika kuwa wakimbizi, kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa.