Rais Tshisekedi asema huenda akagombea muhula wa tatu wa urais, Kongo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138228-rais_tshisekedi_asema_huenda_akagombea_muhula_wa_tatu_wa_urais_kongo
Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amezungumzia uwezekano wa kugombea kiti cha urais kwa muhula wa tatu, akisema atakubali kuendelea kuiongoza nchi hiyo iwapo ataungwa mkono na Wakongo kupitia kura ya maoni.
(last modified 2026-05-07T11:19:40+00:00 )
May 07, 2026 11:13 UTC
  • Félix Tshisekedi
    Félix Tshisekedi

Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amezungumzia uwezekano wa kugombea kiti cha urais kwa muhula wa tatu, akisema atakubali kuendelea kuiongoza nchi hiyo iwapo ataungwa mkono na Wakongo kupitia kura ya maoni.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari siku ya Jumatano, Tshisekedi mwenye umri wa miaka 62 alisisitiza kuwa binafsi hakutaka kuongeza muda wake wa kukaa madarakani zaidi ya kikomo cha mihula miwili kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Kidmeokrasia ya Kongo unaomalizika mwaka wa 2028.

“Sijawahi kufikia kuwania muhula wa tatu, lakini ninawaambia: Kama wananchi wa Kongo wanataka niendelee na muhula wa tatu, nitakubali," amesema Rais wa Felix Tshisekedi.

Ameongeza kuwa: Marekebisho yoyote ya Katiba yanayoruhusu hatua hiyo yatafanyika tu kwa idhini ya umma.

Tshisekedi pia ametahdharisha kuwa mzozo unaoendelea mashariki mwa Kongo unaweza kupelekea kuahirishwa uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika 2028.

Mapigano kati ya wanajeshi wa Kongo na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda yameongezeka katika majimbo yenye utajiri wa madini ya Kivu Kaskazini na Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.