UN yataka kuachiliwa huru wanaharakati wa Global Sumud Flotilla
-
Saif Abukeshek na Thiago Avila
Umoja wa Mataifa umeitaka Israel iwaachilie mara moja wanaharakati wawili wa meli za misaada ya kibinadamu kwa ajili ya watu wa Ukanda wa Gaza wanaoshikiliwa bila mashtaka; na vilevile kuchunguzwa visa vya kuaminika vya kuteswa wanaharakati hao.
Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, Thameen al-Kheetan, amesema kwamba raia wa Uhispania, Saif Abukeshek na Mbrazili Thiago Avila wanaoshikiliwa na Israel, wanapaswa kuachiliwa huru mara moja. Wanaume hao wawili walikuwa miongoni mwa wanaharakati kadhaa waliosafiri kwa meli za msafara wa Global Sumud Flotilla kuelekea Ukanda wa Gaza unaozingirwa na Israel, ambazo zilitekwa nyara na askari wa jeshi la majini la Israel katika maji ya kimataifa karibu na pwani ya Ugiriki tarehe 30 Aprili.
"Sio uhalifu kuonyesha mshikamano na kujaribu kupeleka misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa Palestina huko Gaza, ambayo inahitajika sana," amesema al-Kheetan na kuongeza kuwa, "maelezo ya kutisha ya unyanyasaji mkubwa" dhidi ya mahabusu hao wawili lazima yachunguzwe, na wale waliohusika wafikishwe mbele ya sheria.
Mahakama ya Israel siku ya Jumanne iliongeza muda wa kuwekwa kizuizini Abukeshek na Avila hadi Mei 10. Wanaharakati hao wawili wamekuwa kwenye mgomo wa kula, wakitumia maji pekee, tangu walipokamatwa Alhamisi iliyopita.
Hakuna mashtaka rasmi yaliyowasilishwa dhidi yao, lakini wanakabiliwa na shutuma zinazojumuisha kuwa na uhusiano na "kundi la kigaidi na mawasiliano na mawakala wa kigeni."
Katika tukio la kusikitisha, kundi la kutetea haki za binadamu la Adalah limetangaza kwamba Teresa Regina de Avila e Silva, mama wa Thiago Avila mwenye umri wa miaka 63, amefariki dunia huko Brasilia.
Kundi hilo limeripoti kuwa, askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel walikataa kumruhusu Avila kuzungumza na mama yake kabla ya kifo chake.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa pia ametaka kukomeshwa sera ya Israel ya kuwakamata watu kiholela na kutegemea "sheria za ugaidi zilizofafanuliwa kwa njia isiyoeleweka, ambazo haziendani na sheria za kimataifa za haki za binadamu."