Al Burhan autaka Umoja wa Mataifa kuzuia kumiminwa silaha huko Darfur Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120534-al_burhan_autaka_umoja_wa_mataifa_kuzuia_kumiminwa_silaha_huko_darfur_sudan
Mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Sudan, Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan ameutaka Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba maazimio ya Baraza la Usalama ya kuzuia kuingizwa silaha katika eneo la Darfur la magharibi mwa Sudan na mashambulizi katika mji wa El Fasher yanaheshimiwa kikamilifu.
(last modified 2024-12-24T03:19:25+00:00 )
Dec 24, 2024 03:19 UTC
  • Al Burhan autaka Umoja wa Mataifa kuzuia kumiminwa silaha huko Darfur Sudan

Mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Sudan, Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan ameutaka Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba maazimio ya Baraza la Usalama ya kuzuia kuingizwa silaha katika eneo la Darfur la magharibi mwa Sudan na mashambulizi katika mji wa El Fasher yanaheshimiwa kikamilifu.

Taarifa ya serikali ya Sudan imesema kuwa, al Burhan, ambaye pia ni kamanda mkuu wa Jeshi la Sudan (SAF), alisema hayo jana Jumatatu wakati alipokutana na Mjumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Ramtane Lamamra katika mji wa Bandari ya Mashariki mwa Sudan.

Vilevile amesisitizia dhamira ya serikali yake kufanya kazi na Umoja wa Mataifa katika nyanja zote ikiwa ni pamoja na kulinda usalama wa raia na kuutaka Umoja wa Mataifa kuvishinikiza Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na kulaani ukiukaji wake wa sheria.

Mazungumzo ya Jenerali al Burhan na mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Sudan

 

Kwa upande wake mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa amewaambia waandishi wa habari kuwa katika mazungumzo yake na al Burhan, amethibitisha kuwa Umoja wa Mataifa unazipa kipaumbele kikubwa jitihada za kuutafutia uvumbuzi wa kudumu mgogoro wa Sudan. 

Amebainisha kuwa, vita vya Sudan vilivyodumu kwa takriban miaka miwili sasa vimesababisha watu wengi kuwa wahanga wake na kwamba Umoja wa Mataifa na taasisi zake ziko tayari kushirikiana zaidi na Sudan ili kufikia suluhisho la kudumu la mgogoro wa Sudan na kukomesha mateso ya nchi hiyo na watu wake.

Itakumbukuwa kuwa, tarehe 13 Juni mwaka huu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio linalolitaka kundi la RSF kuacha kuuzingira mji wa El Fasher ambao ni makao makuu ya Jimbo la Darfur Kaskazini. RSF imekuwa ikizingira El Fasher tangu tarehe 10 Mei mwaka huu.