Wapinzani Chad wataka kususiwa uchaguzi, wadai si wa kidemokrasia
Wakati uchaguzi wa wabunge na serikali za mitaa nchni nchini Chad ambao umepangwa kufanyika Disemba 29 unapozidi kukaribia, mjadala mkali unaendelea katika mitaa ya mji mkuu N'Djamena.
Kambi ya upinzani nchini Chad imetoa mwito wa kususiwa uchaguzi huo, wakati chama tawala kikiendesha kampeni kikamilifu. Kampeni za chama tawala zinafanyika kupitia mikutano ya hadhara, hafla na sherehe, kutembelea nyumba kwa nyumba na kampeni za kwenye masoko.
Vyama vya upinzani vinadai kuwa, hatuwezi kushiriki kwenye uchaguzi huu ambao washindi wameshaamuliwa tangu zamani. Kushiriki kwenye chaguzi hizi ni kuhalalisha tu muundo wa utawala wa Chad."
Kambi hiyo ya upinzani inasema kuwa, ni lazima kususia utani na mchezo huu wa kisiasa. Wanawake kutoka chama cha GCAP wamesikika wakiimba: "Usishiriki katika utani huu!"
Kundi la wanawake wapatao 15 waliovaa fulana nyeupe na kofia nyeupe-na-kijani wameonekana kwenye mitaa ya N'Djamena wakisambaza vipeperushi vya kupinga uchaguzi huo na kudai wanawakilisha muungano wa vyama vya upinzani.
Huko nyuma chama cha GCAP kiliwahi kutoa mwito wa kususia kura ya maoni ya katiba iliyoitishwa mwezi Desemba 2023 na uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Mei 2024.
Katika uchaguzi huo, Mahamat Idriss Déby, ambaye alikuwa ametangazwa rais na jeshi baada ya kifo cha babake, alichaguliwa tena kuongoza kwa awamu ya kwanza.
Msemaji wa GCAP, Florence Loardomdemadje, amesema: "Chaguzi zote hizo hazikuwa na uwazi na si halali. Jambo hilo hilo litafanyika tena kwenye uchaguzi ujao."