Maelfu wakimbia vita Sudan, warundikana kwenye mpaka wa Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120590-maelfu_wakimbia_vita_sudan_warundikana_kwenye_mpaka_wa_sudan_kusini
Vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi nchini Sudan vimesababisha zaidi ya watu 80,000 kukimbilia Sudan Kusini katika muda wa chini ya wiki tatu. Wengi wao wamekwama mpakani.
(last modified 2024-12-25T08:45:17+00:00 )
Dec 25, 2024 08:45 UTC
  • Maelfu wakimbia vita Sudan, warundikana kwenye mpaka wa Sudan Kusini

Vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi nchini Sudan vimesababisha zaidi ya watu 80,000 kukimbilia Sudan Kusini katika muda wa chini ya wiki tatu. Wengi wao wamekwama mpakani.

Hayo yamo kwenye taarifa ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) ambalo limeongeza kuwa, wengi wa wakimbizi hao ni wanawake na watoto wadogo ambao wamekimbia mapigano yanayozidi kuongezeka nchini Sudan hasa katika majimbo ya White Nile, Sennar na Blue Nile.

Mmoja wa wakimbizi hao aliyetambuliwa kwa jina moja la Nyarob amesema: “Hali haikuwa salama hata kidogo. Jeshi lilipoingia, kulikuwa na milio ya risasi, na machafuko mengi yalitokea. Mara moja nilichukua watoto wangu na kutembea kwa miguu hadi kwenye mpaka wa Joda pamoja na watu wengine kwa sababu tulihitaji mahali salama kwa watoto wetu.”

Taarifa ya UNHCR imesema kuwa maeneo hayo ya mpakani ikiwemo Joda na vijiji vya jirani yamefurika watu na hayatoshi. Watu wako katika mazingira magumu. Viwango vya utapiamlo vinazidi kuongezeka na ni zaidi ya viwango vya dharura. Maji safi na vyoo hamna kwa kiasi kikubwa suala ambalo linaongeza hatari ya miripuko ya magonjwa.

Silva Alkebeh, Mkuu wa Ugawaji wa Vifaa vya Kilojistiki wa UNHCR amesema: "Mahali hapa wiki mbili zilizopita palikuwa hapana hata mtu mmoja. Tulijenga kituo cha mapokezi ili kuchukua watu mia chache. Kwa sasa, tuna zaidi ya wakimbizi 5,000; wanakaa mpakani na wengi wanaishi kando ya barabara."