Somaliland na Ethiopia zakubaliana kutatua kwa amani mzozo unaoendelea
Maafisa kutoka Jamhuri iliyojitangazia uhuru wake ya Somaliland na wenzao wa Ethiopia wamekubaliana kutatua kwa amani mapigano makali ambayo yametokea katika kipindi cha wiki tatu zilizopita katika kijiji cha mpakani cha Da'awaley.
Taarifa iliyotolewa na utawala wa Somaliland na kuchapishwa na Televisheni ya Taifa ya Somaliland (SNLTV) inayomilikiwa na serikali ilisema makubaliano hayo yamefikiwa kufuatia mazungumzo ya jana huko Jigjiga, mji mkuu wa jimbo la eneo la Somalia la Ethiopia.
Mazungumzo hayo yalifanyika huku kukiwa na mvutano mkali kati ya Somaliland na jimbo la Somalia la Ethiopia kuhusu madai ya kuhusika kwa jeshi la polisi la Liyuu katika mapigano hayo.
Tarehe 25 Disemba, Somaliland ilishutumu jeshi la polisi la Liyuu kwa "kuwaua" wafugaji, kukiuka haki zao za kibinadamu na kusema kuhusika kwao "kunahujumu" mfumo wa utawala katika jimbo la kikanda.
Watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekuwa wakishirikisha picha za kutisha za maiti na mazishi mengi yaliyofanywa kwa waathiriwa.
Mapigano hayo yamekuwa yakitokea ndani na karibu na kijiji cha Dawa'ley katika Wilaya ya Harshin nchini Ethiopia na yameripotiwa kuua zaidi ya watu 100 kulingana na ripoti za vyombo vya habari nchini humo.
Awali mapigano hayo yalihusisha koo zinazohasimiana kutoka Ethiopia na Somaliland, lakini uingiliaji kati wa moja kwa moja wa Polisi wa Liyu - kitengo maalum cha polisi katika Mkoa wa Somalia wa Ethiopia - uliibua hisia na kuikasirisha serikali ya Somaliland.