Wafungwa 6,000 watoroka katika gereza lenye ulinzi mkali Msumbiji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120670-wafungwa_6_000_watoroka_katika_gereza_lenye_ulinzi_mkali_msumbiji
Wafungwa 6000 wametoroka katika jela moja iliyoko karibu na mji mkuu wa Msumbiji, Maputo katika tukio linalodaiwa kupangwa na kuhusishwa na maandamano ya machafuko yaliyozuka baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Oktoba.
(last modified 2024-12-27T07:17:42+00:00 )
Dec 27, 2024 07:17 UTC
  • Wafungwa 6,000 watoroka katika gereza lenye ulinzi mkali Msumbiji

Wafungwa 6000 wametoroka katika jela moja iliyoko karibu na mji mkuu wa Msumbiji, Maputo katika tukio linalodaiwa kupangwa na kuhusishwa na maandamano ya machafuko yaliyozuka baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Oktoba.

Polisi imesema wafungwa walianza kutoroka majira ya mchana siku ya Jumatano baada ya "vurugu" zilizofanywa na "kikundi cha waandamanaji waasi" waliokuwa karibu na gereza kuu la Maputo.

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Msumbiji amesema wafungwa takriban 6,000, wakiwemo 29 waliokuwa wamehukumiwa kwa ugaidi, walitoroka kutoka Gereza Kuu la Maputo siku ya Krismasi wakati wa maandamano yenye vurugu, kufuatia uthibitisho wa ushindi wa chama tawala cha Frelimo katika uchaguzi mkuu uliopita.

 Bernadino Rafael, amesema wafungwa 33 wameaga dunia na wengine 15 walijeruhiwa wakati wa makabiliano na vikosi vya usalama. Maandamano hayo, yaliyofanywa na wafuasi wa mgombea aliyeshindwa Venancio Mondlane, yalisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya polisi na kuanguka kwa ukuta wa gereza.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Msumbiji Pascoal Ronda ameyahusisha machafuko hayo na mzozo wa matokeo ya uchaguzi, huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akitoa wito wa mazungumzo na kukomesha vurugu. Wafungwa wengi waliotoroka tayari wamekamatwa tena.

Tukio la wafungwa kutoroka jela nchini Msumbiji limezuka huku nchi hiyo ikishuhudiwa wimbi la maandamano mapya kufuatia tangazo la Jumatatu la Mahakama ya Kikatiba lililothibitisha kwamba Daniel Chapo wa chama tawala cha Frelimo alikuwa ameshinda uchaguzi wa rais wa Oktoba uliogubikwa na mgogoro.