Mamlaka Kenya zakanusha kuwateka wakosoaji wa serikali ya Ruto
Idara ya upelelezi nchini Kenya, DCI imekanusha madai kwamba, inahusika kwenye visa vya utekaji na kupotezwa kwa wanaharakati wa mitandaoni wanaokosoa uongozi wa rais William Ruto.
Kwa mujibu wa taarifa ya idara ya upelelezi nchini Kenya, DCI iliyosambazwa kwa vyumba vya habari saa chache zilizopita, taasisi hiyo imesema kamwe haijahusika na utekaji wa wanaharakati kama ilivyodaiwa.
Taarifa hiyo ilizuka baada ya Seneta wa kaunti ya Busia, Okiya Omtatah kudai kuwa, mwanaharakati Kibet Bull almaarufu Yoko, alitekwa na watu waliotumia gari jeupe aina ya Subaru Forester lililokuwa na nambari bandia ya usajili. Kisa hicho kilitokea baada ya mkutano kati ya Seneta wa Busia Okiya Omtatah na Kibet Bull katika eneo la Upper Hill jijini Nairobi.
Hayo yanajiri masaa kadhaa baada ya Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNCHR) kukanusha ripoti ya Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja kwamba hakuna Wakenya waliotekwa nyara nchini humo ikisema, katika mwezi huu wa Desemba pekee, watu saba hasa watumiaji wa mitandao ya kijamii wametekwa nyara; na kufikia sasa, sita hawajulikani waliko.
Tangu mwanzoni mwa wiki,wanaharakati kadhaa waliripotiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha nao ni Billy Mwangi, Peter Muteti, Bernard Kavuli, na Naomi kutokea kaunti za Embu, Nairobi na Kajiado.Wanne hao wamekuwa wakitoa maoni yao mtandaoni.