Wahamiaji 69 wafariki baada ya boti yao kuzama karibu na Morocco
Takriban watu 69, wakiwemo wahamiaji 25 kutoka Mali, wamekufa baada ya mashua yao kuzama katika pwani ya Morocco.
Hayo yamethibitiwa na Waziri wa Raia wa Mali Wanaoishi Nje ya Nchi (Diaspora), Mossa Ag Attaher ambaye amesema katika taarifa kwamba boti ya muda ambayo wahamiaji walikuwa wakisafiria ilizama Disemba 19 na kupelekea makumi ya watu kufariki dunia wakiwemo raia wa Mali.
Amesema: "Vijana 25 wa Mali kwa bahati mbaya wametambuliwa rasmi kuwa ni miongoni mwa waathiriwa."
Hayo yanaripotiwa wakati ambao uchunguzi umebaini kuwa zaidi ya wahamiaji 10,000 wamefariki dunia au kupotea mwaka huu wa 2024 unaomalizika wakati wakijaribu kufika Uhispania kwa njia ya Bahari.
Ripoti iliyotolewwa na shirika lisilo la kiserikali la Caminando Fronteras inaonyesha kuwa, zaidi ya wahamiaji 10,000 wamefariki dunia au kupotea wakiwa katika juhudi za kuelekea nchini Uhispania kwa njia ya majini.
Kwa mujibu wa shirika hilo idadi hiyo imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 50 ikilinganishwa na mwaka uliopita na kubwa zaidi tangu mwaka 2007.
Ongezeko hilo la asilimia 58 linajumuisha watoto 1,538 na wanawake 421, kundi la kutetea haki za wahamiaji Caminando Fronteras limesema katika ripoti yake ambayo imeangazia matukio ya kipindi cha tangu Januari 1 hadi Disemba 5, 2024.
Shirika hilo limehesabu wastani wa wahamiaji 30 waliofariki dunia kwa siku, zaidi ya wastani wa vifo18 kwa siku mwaka 2023.
Kundi hilo limekusanya takwimu zake kutokana na simu za dharura walizowekewa wahamiaji kwenye meli zilizo katika shida ili kuomba msaada, familia za wahamiaji waliotoweka na takwimu rasmi kutoka idara za uokoaji.
Kadhalika limesema idadi ya vifo iliongezeka kutokana na kutumia boti chakavu na njia hatari pamoja na uwezo duni wa huduma za uokoaji baharini.