Jeshi la DRC lamkamata askari wa Rwanda, taharuki yatanda
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambalo kwa kifupi hujulikana kama FARDC limetangaza kuwakamata askari wa kikosi maalum cha Jeshi la Rwanda wakati wa mapigano huko wilayani Lubero mkoani Kivu Kaskazini huku hali ya taharuki ikitanda katika eneo la mpaka baina ya nchi hizo mbili
Jeshi la DRC linasema askari huyo aliyekamatwa alithibitisha uwepo wa wanajeshi wa Rwanda kwenye ardhi ya DRC kwa lengo la kuwasaidia waasi wa M23. Taarifa ya FARDC imesema askari huyo ambaye jina lake limetajwa kuwa ni Hakizimana Iradukunda Jean, ni miongoni mwa wanajeshi wengine wa Rwanda waliokamatwa Jumamosi kati ya vijiji vya Mambasa na Ndoluma wakati wa mapigano baina ya Jeshi la DRC na waasi wa M23 wilayani Lubero.
Serikali ya DRC inaishutumu Rwanda kwa kuwapeleka zaidi ya wanajeshi 4,000 katika eneo lake, hasa upande wa jimbo la Kivu Kaskazini, ambako mapigano yameongezeka katika miezi ya hivi karibuni.
Hayo yanajiri baada ya Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kutangaza kuwa, 'limedungua' ndege sita zisizo na rubani za Kamikaze za jeshi la Rwanda katika mji wa Mambasa eneo la Lubero katika Mkoa wa Kivu Kaskazini.
Mapigano makali kati ya waasi wa M23 na jeshi la serikali ya Kongo likishirikiana na wanajeshi wa Kikosi cha Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC yamesababisha wimbi jipya la wakimbizi wa ndani mashariki mwa DRC.
Kongo DR imekuwa ikimtuhumu jirani yake Rwanda kuwa inaliunga mkono kundi la waasi wa M23, madai ambayo yamekanushwa na Kigali.
Mazungumzo kati ya viongozi wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili kumaliza mzozo wa mashariki mwa DRC hayakufanyika kati kati ya mwezi huu kama ilivyotarajiwa kutokana na mivutano kati ya serikali za nchi hizo mbili.
Kundi la waasi wa M23 limeteka maeneo kadhaa mashariki mwa DRC na kusababisha maelfu ya watu kuhama makazi yao na kuchochea mzozo wa kibinadamu.
Kulikuwa na matumaini kwamba mkutano ambao ungesimamiwa na Rais wa Angola Joao Laourenco, mpatanishi aliyeteuliwa na Umoja wa Afrika, ungefikia makubaliano ya kumaliza mzozo wa mashariki mwa Congo.
Lakini mkuu wa ofisi ya mawasiliano kwenye ofisi ya rais wa Angola alisema mazungumzo hayatafanyika.