Baraza la Usalama laidhinisha kikosi kipya cha kulinda amani nchini Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120708-baraza_la_usalama_laidhinisha_kikosi_kipya_cha_kulinda_amani_nchini_somalia
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana, Ijumaa, liliidhinisha uamuzi wa kupeleka ujumbe mpya wa Umoja wa Afrika nchini Somalia, ambao utachukua nafasi ya kikosi kingine cha umoja huo, kuanzia mwanzoni mwa mwaka ujao, kwa lengo la kupambana na wanamgambo wa Al-Shabaab.
(last modified 2024-12-28T04:02:53+00:00 )
Dec 28, 2024 04:02 UTC
  • Baraza la Usalama la  UN
    Baraza la Usalama la UN

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana, Ijumaa, liliidhinisha uamuzi wa kupeleka ujumbe mpya wa Umoja wa Afrika nchini Somalia, ambao utachukua nafasi ya kikosi kingine cha umoja huo, kuanzia mwanzoni mwa mwaka ujao, kwa lengo la kupambana na wanamgambo wa Al-Shabaab.

Kikosi hicho kipya kinajulikana kama Kikosi cha Kusaidia na Kuimarisha Utulivu cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AUSSOM), na kitafanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja kamili kikichukua nafasi ya Misheni ya Mpito ya Umoja wa Afrika (ATMIS), ambayo iliidhinishwa na Baraza la Usalama mnamo 2022 kwa ajili ya kupambana na kundi la al Shabaab hadi mwisho wa 2024.

Baraza la Usalama limeidhinisha uamuzi wa kuunda kikosi hicho kipya kwa wingi wa mataifa 14 kati ya nchi 15 wanachama, huku nchi moja ambayo ni Marekani, ikisusia kupiga kura.

Chini ya azimio hilo la Umoja wa Mataifa, ujumbe huo utasaidia vikosi vya jeshi la Somalia katika kuimarisha usalama kwa ajili ya michakato ya kisiasa katika ngazi zote, kulingana na mpango wa kitaifa wa kurejesha utulivu.

Somalia, mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, inasumbuliwa na miongo kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, uasi wa umwagaji damu unaofanywa na kundi la al-Shabaab lenye mafungamano na kundi la kigaidi la al-Qaida na majanga ya mara kwa mara ya hali ya hewa.