Rais wa Algeria akosoa Ufaransa kuhusu historia yake ya ukoloni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120788-rais_wa_algeria_akosoa_ufaransa_kuhusu_historia_yake_ya_ukoloni
Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune amekosoa vikali Ufaransa kuhusu athari za utawala wake wa kikoloni zilizosalia nchini humo.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Dec 30, 2024 04:21 UTC
  • Rais wa Algeria akosoa Ufaransa kuhusu historia yake ya ukoloni

Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune amekosoa vikali Ufaransa kuhusu athari za utawala wake wa kikoloni zilizosalia nchini humo.

Tabboune ameyasema hayo mbele ya mabunge yote mawili ambapo alibainisha mafanikio ya duru yake ya kwanza ya urais tokea 2019 hadi 2024. Katika kikao hicho  Tebboune ameisisitiza kwamba Algeria inataka Ufaransa itambue uhalifu wake wakati wa kipindi cha ukoloni kutoka mwaka 1830-1962. Amesisitiza kwamba "Algeria haitafuti fidia ya kifedha bali inatafuta heshima ya mababu zetu."

Ameongeza kuwa: "Idadi ya mashujaa wa Algeria katika kipindi chote cha miaka 132 ya ukoloni ni milioni 5.6, na hakuna kiwango chochote cha pesa kinachoweza kufidia kupoteza shujaa hata mmoja wakati wa mapambano ya silaha."

Tebboune alielezea ukatili uliofanywa na jeshi la kikoloni la Ufaransa, hasa chini ya Jenerali Thomas Robert Bugeaud, ambaye alimuelezea kama "muuaji wa kimbari." Pia alisema kwamba Ufaransa inaendelea kushikilia fuvu 500 za Waalgeria waliokatwa vichwa katika karne ya 19 na kupelekwa Paris, ambapo ni 24 tu zimepatikana hadi sasa.

Kauli hiyo imekuja huku kukiwa na  mgogoro mkubwa wa kisiasa kati ya Algeria na Ufaransa ambao umesababisha kurejea nyumbani balozi wa Algeria aliyekuwa Ufaransa na kuitwa kwa balozi wa Ufaransa kujieleza katika wizara ya mambo ya nje ya Algeria..

Algeria inasema Ufaransa inahusika "matendo ya uhasama na ujasusi kwenye ardhi ya Algeria."

Katika masuala ya ndani, Tebboune alitangaza mipango ya kuanzisha mazungumzo na vyama vya kisiasa mapema mwaka ujao ili kuimarisha  umoja wa ndani. Mazungumzo haya yanatarajiwa kuwa jumuishi na ya kina, yakihitimishwa na kuanzishwa kwa sheria mpya zinazodhibiti vyama vya kisiasa na jumuiya za kiraia.