Polisi: Watu 600 wametoroka kizuizini Sudan Kusini
(last modified Thu, 23 Jan 2025 07:38:31 GMT )
Jan 23, 2025 07:38 UTC
  • Polisi: Watu 600 wametoroka kizuizini Sudan Kusini

Polisi nchini Sudan Kusini imesema watu 600 waliokuwa wakizuiliwa baada ya kukamatwa kwa kushiriki maandamano ya ghasia na uporaji wa biashara wametoroka katika jela ya kijeshi katika mji mkuu Juba.

Msemaji wa Polisi ya Sudan Kusini, Kanali John Kassara Koang Nhial alisema jana Jumatano kuwa, maafisa usalama walifyatua risasi hewani walipokuwa wakiwafuata waliotoroka, na kufanikiwa kuwakamata tena watu 410. Kwa mujibu wa ripoti ya tovuti ya Redio Tamazuj, maafisa wa polisi wanawasaka wafungwa wengine waliotoroka jela.

Wiki iliyopita, maandamano ya ghasia yalizuka nchini Sudan Kusini baada ya video za kutisha kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, zikionyesha raia wa Sudan Kusini waliouawa huko Wad Madani, mji mkuu wa jimbo la Al-Jazira.

Wakati huo huo, Sudan Kusini imetangaza kufunga mitandao ya kijamii kama Facebook na Tiktok kwa muda wa miezi mitatu, kwa lengo la kudhibiti ghasia nchini humo.

Ikumbukwe kuwa, raia 16 wa Sudan waliuawa wakati wa maandamano ya wiki iliyopita nchini humo kama sehemu ya malalamiko yaliyotokea baada ya mauaji ya watu wa Sudan Kusini katika jimbo la Al-Jazira nchini Sudan.

Serikali ya Sudan ilitoa amri ya kutotoka nje kote nchini humo wiki iliyopita, kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi saa 12 asubuhi kwa saa za eneo hilo ili kudhibiti uporaji na vurugu.