Nigeria yachunguza mripuko mwingine wa lori la mafuta ulioua 18
Mamlaka za Nigeria zimeanzisha uchunguzi baada ya watu 18 kuthibitishwa kufariki dunia kwenye mripuko wa lori la mafuta ya petroli.
Vyanzo vya habari vimeiambia Anadolu kwamba, magari mengine sita yaliteketea wakati lori la mafuta lilipoanguka, lilipokuwa likishuka kwenye barabara ya mwendokasi yenye milima mingi katika Jimbo la Enugu, kusini mashariki mwa nchi.
Rais Bola Tinubu ameeleza kusikitishwa kwake na taarifa za mripuko huo mbaya wa lori la mafuta ya petroli ulioua idadi kubwa ya watu katika Jimbo la Enugu. Rais Tinubu amewataka watumiaji wa barabara, hasa wasafirishaji wa mafuta, kuzingatia kanuni za trafiki zilizowekwa.
Katika taarifa, Mshauri Maalum wa Habari na Mikakati wa Rais, Bayo Onanuga jana Jumapili alisema Rais Tinubu alitoa salamu za rambirambi kwa serikali na watu wa Jimbo la Enugu, pamoja na familia za walioaga dunia, na kuwatakia afueni ya haraka majeruhi wa mkas huo.
Haya yanajiri wiki moja baada ya watu 98 kuaga dunia katika Jimbo la Niger nchini Nigeria, katika tukio jingine la mripuko mkubwa wa lori la mafuta. Hilo lilikuwa tukio la pili la ajali ya aina hii ndani ya miezi mitatu iliyopita.
Mnamo Oktoba mwaka jana, matukio kama hayo yalitokea katika Jimbo la Jigawa kaskazini mwa nchi, na kuua zaidi ya watu 170. Aidha mwanzoni mwa mwezi Septemba pia, makumi ya watu walipoteza maisha baada ya lori la mafuta kuripuka kaskazini mwa Nigeria.
Limekuwa jambo la kawaida huko Nigeria ambapo watu wengi huhatarisha maisha yao kwa kukimbilia malori yanayopinduka ili kuchota mafuta hasa ukizingatia kupanda kwa bei ya mafuta nchini humo, tangu serikali ilipositisha mpango wake wenye gharama kubwa wa kufadhili ruzuku ya gesi.