Human Rights Watch: Mzozo DRC unaweza kuleta maafa ya kibinadamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121946-human_rights_watch_mzozo_drc_unaweza_kuleta_maafa_ya_kibinadamu
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetahadharisha kuhusiana na mapigano yanayoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kueleza uwezekano wa kutokea maafaa ya kibinadamu.
(last modified 2025-01-26T23:15:58+00:00 )
Jan 26, 2025 23:15 UTC
  • Human Rights Watch: Mzozo DRC unaweza kuleta maafa ya kibinadamu

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetahadharisha kuhusiana na mapigano yanayoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kueleza uwezekano wa kutokea maafaa ya kibinadamu.

Mtafiti mkuu wa shirika la HRW barani Afrika, Clementine de Montjoye, amesema hali inayowakabili raia wa Goma inazidi kuwa ya hatari na mahitaji ya kibinadamu ni makubwa. Kwenye taarifa yake shirika hilo limetahadharisha kuhusu matokeo mabaya yatakayowafika watu katika eneo hilo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa upande wake Umoja wa Afrika umehimiza "kusitishwa mara moja" kwa mapigano makali mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ametoa mwito kwa vikosi vya Rwanda kuondoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na kuacha kuwasaidia wapiganaji wa M23 wanaosonga mbele katika mji wa Goma.

Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) inalaani mauaji ya vikosi vyake yaliyotekelezwa na M23 mashariki mwa DRC, na kutaja mashambulizi hayo kama "kitendo cha uchokozi."

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kukata uhusiano wa kidiplomasia na Rwanda huku mapigano kati ya waasi wanaoungwa mkono na Rwanda na vikosi vya serikali yakiendelea kuzunguka mji muhimu wa mashariki wa Goma.

Mapigano hayo yamesababisha walinda amani 13 na wanajeshi wa kigeni kuuawa na maelfu ya raia kuyahama makaazi yao.