Takriban watu 56 wameuawa Sudan huku mapigano yakiendelea Khartoum
Mashambulio ya mizinga na ya anga yalisababisha vifo vya takriban watu 56 jana Jumamosi katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum. Haya yameelezwa na duru za hospitali na wanaharakati wa Sudan.
Vikosi vya jeshi la Sudan na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) wanapigana kuwania madaraka tangu mwezi Aprili mwaka 2023. Mapigano kati ya pande mbili hizo yamepamba moto tangu mwezi uliopita ambapo jeshi la Sudan limezidisha mashambulizi yake dhidi ya wanamgambo wa RSF ili kudhibiti maeneo yote ya mji mkuu, Khartoum na miji yake dada ya Omdurman na Khartoum ya Bahri.
Ripoti zinasema, mashambulizi ya mizinga na ya anga ya kikosi cha RSF yameuwa watu 54 katika soko lenye watu wengi katika mji wa Omdurman, na habari zinasema kuwa hospitali ya al Nao katika mji huo imejaa majeruhi wa hujuma hiyo.
Wanamgambo wa RSF walishambulia katikati ya soko la mboga na kuua na kujeruuhi idadi kubwa ya watu.
Inafaa kukumbusha hapa kuwa jeshi la Sudan mwezi uliopita lilizidhibiti tena kambi kadhaa za kijeshi huko Khartoum, ikiwa ni pamoja na makao yake makuu na hivyo kuwarejesha nyuma wanamgambo wa RSF baada ya kukwama kwa miezi kadhaa huko Khartoum.