Nairobi, mwenyeji wa Mkutano wa Ustaarabu wa Iran A/Mashariki
(last modified Fri, 07 Feb 2025 07:55:21 GMT )
Feb 07, 2025 07:55 UTC
  • Nairobi, mwenyeji wa Mkutano wa Ustaarabu wa Iran A/Mashariki

Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya jana Alkhamisi kilikuwa mwenyeji wa mkutano wa Ubalozi wa Iran wenye kaulimbiu inayosema "Kupekua Ushawishi wa Ustaarabu na Utamaduni wa Kiajemi kwa jamii za Afrika Mashariki."

Fatuma Mohammed Achani, Gavana wa Kaunti ya Kwale, pwani ya Kenya ambaye alihudhuria mkutano huo amesema, Wazawa wa Shirazi bado wanaishi katika eneo hilo, na waliboresha eneo hilo kwa mchanganyiko wao wa utamaduni wa Kiajemi na Waswahili, ambao ulizalisha lahaja ya Shirazi.

Naye Ali Gholampour, Balozi wa Iran mjini Nairobi ameeleza bayana kuwa, baadhi ya mitishamba, viungo, na vyombo vililetwa katika eneo hili na Waajemi, na ushawishi wao bado unaonekana hadi leo hii, hasa katika maeneo ya pwani.

Kwa upande wake, Ali Pourmarjan, Mwambata wa Utamaduni katika Ubalozi wa Iran nchini Kenya amesema, athari za jamii ya Washirazi wa Uajemi mara nyingi huachwa ingawa mchango wao kwa Afrika ni mkubwa na unastahili kufanywa sehemu ya utambulisho wa watu.

Ustaarabu wa Uajemi, ulioletwa Afrika Mashariki na Washirazi na Mabulushi wa Iran katikati ya karne ya 18, ulisababisha utambulisho wa kitamaduni ulioboreshwa, kuimarika kwa uchumi, na mshikamano wa kijamii. Hii inaendelea kuchangia uelewa wa kina wa maingiliano ya kihistoria na ya kisasa kati ya mataifa ya Iran na Afrika Mashariki.

Utafiti wa chembe chembe za vinasaba unaonyesha kuwa, Waswahili wa Ukanda wa Pwani Afrika Mashariki wana asili ya Iran. Utafiti huo uliofanywa kutoka kwa watu 80 waliozikwa katika karne za nyuma katika miji ya uswahili pwani ya Afrika Mashariki ulifichua kwamba watu hao walikuwa na asili ya Kiafrika na kutoka Asia.