Mali: Tunawasaka wanamgambo wenye silaha waliouwa watu zaidi ya 25
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122526-mali_tunawasaka_wanamgambo_wenye_silaha_waliouwa_watu_zaidi_ya_25
Jeshi la Mali limeahidi kuwasaka "magaidi" waliohusika na shambulio la kikatili dhidi ya msafara mkubwa uliokuwa ukielekea kwenye mgodi wa dhahabu nchini humo.
(last modified 2025-02-09T23:11:49+00:00 )
Feb 09, 2025 23:11 UTC
  • Mali: Tunawasaka wanamgambo wenye silaha waliouwa watu zaidi ya 25

Jeshi la Mali limeahidi kuwasaka "magaidi" waliohusika na shambulio la kikatili dhidi ya msafara mkubwa uliokuwa ukielekea kwenye mgodi wa dhahabu nchini humo.

Maafisa wa Mali wameeleza kuwa, askari jeshi wa nchi hiyo na wengine kadhaa kutoka kundi la Wagner walikuwa wakilisindikiza kundi la watu ambao aghalabu yao walikuwa raia wa kigeni kuelekea katika mgodi wa madini wa Intahaka, eneo kuu la uchimbaji dhahabu kaskazini mwa Mali wakati walipovamiwa ghafla na watu waliokuwa na silaha. 

Wavamizi hao walitekeleza hujuma hiyo wakati msafara wa makundi kadhaa ya magari yakiwa njiani katika kijiji cha Kobe; eneo ambalo linajulikana kwa uhalifu wa wanamgambo wenye silaha. Aidha mashambulizi kadhaa yamejiri katika eneo hilo katika miezi ya karibuni. 

Afisa wa ngazi ya Jenerali wa jeshi la Mali ambaye hakutaja jina lakelitajwe ameviambia vyombo vya habari kuwa magaidi waliwashambulia kwa makusudi raia wa kawaida wakati walipokabiliana nao na kwamba wanaendelea kuwasaka magaidi waliohusika na mauaji ya raia hao wa kigeni.

Jeshi la Mali limetangaza kuwa raia 25 wameuawa na wengine 13 kujeruhiwa; aghalabu yao wakiwa ni wachimba madini vijana wa nchi za kigeni. "Miili ya magaidi 19 pia imepatikana katika eneo la tukio," imeeleza taarifa ya jeshi la Mali.

Mali  ni miongoni mwa wazalishaji wakuu wa madini ya dhahabu barani Afrika, ingawa uzalishaji umeshuka kutokana na ukosefu wa usalama.