"Maharamia" warejea kwa nguvu Somalia, wateka nyara meli ya uvuvi
Watu wanaoshukiwa kuwa mo maharamia wameteka nyara meli ya uvuvi iliyokuwa na bendera ya Yemen karibu na Eyl, kaskazini mwa Somalia.
Vyombo mbalimbali vimeripoti habari hiyo na kusema kuwa, juhudi mbalimbali zimeanza kuhakikisha meli hiyo inakombolewa na kusikiliza watekaji wanataka nini.
Vyombo hivyo vya habari vimeandika: Maharamia wa Kisomali waliojihami kwa silaha wametumia boti zinazokwenda kwa kasi kuivamia na kuiteka meli hiyo ya uvuvi.
Katikati ya mwezi uliopita wa Januari, Ofisi ya Kimataifa ya Biashara ya Baharini (IMB) ilitoa mwito wa kuwepo umakini katika fukwe za Somalia na Ghuba ya Aden, kwani uharamia bado unaendelea kuwa tishio.
Mwaka jana, matukio manane ya uharamia yaliripotiwa kutokea kwenye bahari ya ukanda wa pwani wa Somalia.
Taarifa hiyo imesema kuwa, maharamia wa Kisomali waliiteka meli hiyo ya uvuvi yenye bendera ya Yemen kwenye pwani ya mji wa Eyl wa kaskazini mashariki mwa jimbo la Puntland la Somalia siku ya Jumapili.
Maafisa wa jimbo la Puntland la Somalia wamethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, meli hiyo, ilipewa leseni na mamlaka ya Puntland na ilitekwa nyara na watu wenye silaha na hadi hivi sasa haijulikani ilipo.
Hili ni tukio la kwanza la uharamia katika pwani ya Somalia mwaka huu, kufuatia kuibuka tena mashambulizi hayo mwaka jana. Mwishoni mwa mwaka jana, meli moja ya uvuvi ya China itekwa nyara na kukombolewa kwa kulipwa kikomboleo kilichotakiwa na maharamia.