Watu 108 waaga dunia kwa ugonjwa wa kipindupindu nchini Angola
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122632-watu_108_waaga_dunia_kwa_ugonjwa_wa_kipindupindu_nchini_angola
Watu karibu 108 wamefariki dunia nchini Angola kutokana na mlipuko wa kipindupindu tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Hiyo ni kulingana na taarifa ya wizara ya afya ya nchi hiyo.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Feb 12, 2025 03:42 UTC
  • Watu 108 waaga dunia kwa ugonjwa wa kipindupindu nchini Angola

Watu karibu 108 wamefariki dunia nchini Angola kutokana na mlipuko wa kipindupindu tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Hiyo ni kulingana na taarifa ya wizara ya afya ya nchi hiyo.

Takwimu hizi zimetolewa wakati huu idadi ya vifo ikiripotiwa kuongezeka katika siku za hivi karibuni.

Hadi kufikia sasa, visa 3,147 vya ugonjwa wa kipindupindu vimethibitishwa kwenye taifa hilo tangu tarehe saba ya mwezi Januari.

Kulingana na Wizara ya Afya ya Angola, karibu nusu ya visa vyote vya maambukizo ya kipindupindu vimeripotiwa katika mji mkuu Luanda. Mamlaka inasema walioambukizwa ni wa umri kati ya miaka miwili hadi 100.

Watu 48 wamethibitishwa kufariki mjini Luanda na wengine 43 katika eneo la Bengo lililo katika mpaka na mji mkuu.

Wizara ya Afya ya Angola imetaja changamoto inazokabiliana nazo katika kudhibiti mripuko huo, hususan usafi wa mazingira katika maeneo yaliyoathirika zaidi na ukosefu wa mifumo ya maji safi ya kunywa katika maeneo hatarishi.

Wakati huo huo, mwezi uliopita Malawi ilizindua mpango wa miaka 5 wa kudhibiti kipindupindu ambao unalenga kupunguza kiwango cha matukio ya kila mwaka ya ugonjwa huo kwa asilimia 90 na kufikia kiwango cha chini kabisa cha vifo ifikapo mwaka 2030.

Dalili za kipindupindu zinazofahamika zaidi ni kuharisha sana na kutapika, ambazo zinaweza kusababisha upungufu mkubwa wa maji mwilini.

Matibabu ya kipindupindu yanahusisha zaidi kurejesha maji mwilini na pengine matumizi ya antibiotiki.

Kipindupindu kwa kawaida hutokea katika maeneo yenye ukosefu wa usafi, upatikanaji mdogo wa maji safi ya kunywa, na miundombinu duni ya usafi.